Mkutano wa pili wa Bunge la 12 unaanza leo jijini Dodoma ambapo wabunge watauliza maswali na kuchangia hoja mbalimbali ikiwa ni mara ya kwanza kufanyika bila kuwa na kambi ya upinzani tangu kuanza kwa mfumo wa vyama vingi.

Spika wa Bunge, Job Ndugai  jana Februari 1, 2021 aliongoza kikao cha kamati ya uongozi kilichofanyika katika ofisi za Bunge na kujadili maelezo kuhusu majukumu ya kamati ya uongozi.

Pamoja na mambo mengine, wabunge wanatarajia kuwa kupitia tathimini ya utekelezaji wa Mpango wa pili wa Maendeleo ya Taifa kwa miaka mitano, 2016/17-2020/21 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano, 2021/22-2025/26.

Shughuli nyingine zinazotarajiwa kufanyika ni kupitia Mpango wa Maendeleo ya Taifa wa mwaka mmoja 2021/22 na mwongozo wa kuandaa Mpango na Bajeti ya Serikali kwa mwaka wa fedha 2021/22 ikiwemo Taarifa ya utekelezaji wa Bajeti ya Serikali na Sheria ya Fedha kwa kipindi cha nusu mwaka wa 2020/21.

Hata hivyo hili ndilo Bunge lenye idadi ndogo ya wapinzani ambao hawakufikia asilimia 12.5 zinazotakiwa kuunda kambi ya walio wachache bungeni, tofauti na Bunge la 11 na 10 ambayo yalikuwa na idadi kubwa ya wapinzani.

Kuanza kwa mkutano huu kutatoa taswira halisi ya wabunge 19 ambao wamefukuzwa uanachama ndani ya chama hicho kikuu cha upinzani nchini licha ya taarifa kuwa shauri lao bado linashughulikiwa ndani ya chama.

Kwa upande wa wabunge wa CCM ambako kuna sura nyingi mpya, wabunge wataanza kurusha karata zao kwenye mijadala na maswali kwa mawaziri wapya.

Itakumbukwa, wakati Rais Magufuli aliwataka wabunge kutounga mkono kila jambo badala yake wakosoe inapobidi ila wawe wenye kutoa hoja wakati akizindua Bunge la 12, Novemba mwaka jana.

“Katika hilo, kwa upande wetu Serikali, tunaahidi kutoa ushirikiano wa kutosha kwa Bunge hili ili kuliwezesha kutimiza majukumu yake ipasavyo,” alisema Rais Magufuli.

 

 

Azam FC: Tutaifunga TP Mazembe
Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 2, 2021