Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC kesho Jumatano (Februari 03) watasafiri kuelekea mkoani Dodoma, kwa ajili ya mchezo wa kiporo dhidi ya Dodoma Jiji FC, ambao utachezwa Februari 04, Uwanja wa Jamhuri.

Simba SC inayonolewa na kocha Didier Gomez Da Rossa itaanza safari ya kuelekea mjini humo, ikiwa na deni la kuendeleza wimbi la ushindi kwenye michezo ya Ligi Kuu Tanzania Bara, ambayo ilisimama kupisha Fainali za Mataifa Bingwa ya Afrika ‘CHAN’.

Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano ya Simba SC Haji Sunday Ramadhan Manara amesema watakapokuwa mjini Dodoma, kikosi chao pamoja na viongozi watapata nafasi ya kwenda bungeni kupeleka kombe la ubingwa wa Simba Super Cup, pamoja na kupewa baraka na wabunge kwa ajili ya kuiwakilisha nchi kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hatua ya makundi.

“Tutaondoka asubuhi Jumatano ili kwenda Dodoma kwa ajili ya mchezo wetu wa Ligi Kuu Bara dhidi ya Dodoma Jiji FC ambao utachezwa Uwanja wa Jamhuri Dodoma, lakini pia tutapata nafasi ya kwenda bungeni Februari 3.”

“Bungeni tutakwenda kupata baraka za Wabunge wetu hasa ukizingatia kwamba tunakwenda kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika. Februari 5 baada ya mchezo wetu tutarudi Dar kwa ajili ya maandalizi ya mchezo wetu wa ligi dhidi ya Azam FC,” amesema.

Mabingwa hao wa Simba Super Cup mchezo wao wa mwisho ilikuwa ni Januari 31 ambapo walicheza na TP Mazembe.

Dakika 90 zilikamilika kwa sare ya bila kufungana Uwanja wa Mkapa ambapo kikosi cha Gomes kilibadilika tofauti na kile ambacho kilishinda mabao 4-1 dhidi ya Al Hilal, Uwanja wa Mkapa.

Kwenye mchezo wa kwanza kiungo mshambuliaji Miraji Athuman alianza benchi ila kwenye mchezo dhidi ya TP Mazembe alianza kikosi cha kwanza.

JPM aitaka Wizara ya Sheria kushugulikia haraka ajira 200
Biden atishia kuiwekea vikwazo Myanmar