Kufuatia mauaji ya watu 32 yaliyotekelezwa na kundi la wezi wa mifugo wanaojiita ‘Dahalo’ katika Kijiji kimoja cha nchini Madagaska, Polisi nchini humo imeanzisha msako wa kuwabaini wahusika ili wakamatwe na kufikishwa katika vyombo vya Sheria.

Wezi hao wa mifugo, waliwachoma moto watu 32 wakiwa hai, wakiwemo wanawake na watoto 15 ambapo siku ya Ijumaa Julai 29, 2022 pia walichoma moto nyumba katika kijiji cha Ambolotarakely, kilichopo kilomita 75 kaskazini mwa mji mkuu wa nchi hiyo, Antananarivo.

Vyombo vya Habari nchini humo, vimeripoti kuwa katika eneo la gendarmerie watu watano wanaoshukiwa kuhusika na mauaji hayo walikamatwa siku ya Jumatatu Agosti 1, 2022 na kwamba bado msako unaendelea, huku helikopta za kijeshi na askari wa ardhini wakiwatafuta waliohusika.

Waziri wa Ulinzi wa Madagascar, Jenerali Richard Rakotonirina amesema, “Ni kitendo cha ghasia zisizokubalika, na lazima wahusika wakamatwe na waadhibiwe vikali sana, tunawasaka wahalifu hao mpaka wapatikane.”

Hata hivyo, Jeshi la polisi wamelaani mauaji hayo yaliyofanywa na wezi wa ng’ombe wanaofahamika kwa jina la dahalo, ingawa bado haijafahamika wazi kuhusu dhamira ya wahusika katika kutenda ukatili wa kiwango hicho.

Kwa mujibu wa rais wa Tume Huru ya Kitaifa ya Haki za Kibinadamu (CNIDH), Seth Andriamarohasina amesema vikosi vya usalama vilikuwa vikishika doria katika kijiji hicho, ambacho kiko kwenye kilima kidogo mwendo wa saa 10 kutoka kituo cha Polisi cha karibu.

“Ni kijiji cha mizimu sasa, maana wakazi wote wameondoka kwa kuhofia hao wanaojiita dahalo, huu ni ukatili wa ajabu sana kuuwa ahata watoto angalia watu waliouawa nao hawana hatia ni lazima kuwakamata hawa watu” alisema Andriamarohasina.

Wizara ya ulinzi nchini Madagascar imesema uchunguzi wa awali unaonesha kuwa mzozo wa ardhi umehusisha mauaji hayo na kuleta ghasia na kwamba kitendo hicho kilichopangwa kabla ya kutekelezwa ili kufanikisha mauaji hayo.

Makinda: Sensa siyo zoezi la siku moja
Kopafasta yaibua tabasamu kwa Taifa huduma ya 'mafuta kadi'