Waliokosa mikopo elimu ya juu wapewa siku 14

By dar24.com - Mon Oct 28, 5:10 am

noti10000_300_148 (1)

WANAFUNZI 1,107 wa masomo ya kipaumbele waliokosa mkopo kutokana na fomu zao za maombi kuwa na dosari, wamepewa muda hadi Novemba 6 mwaka huu, wawe wameshasahihisha fomu hizo. Wanafunzi hao wanaonufaika ni wa ualimu wa hisabati (20), ualimu wa sayansi (164), wanafunzi wa sayansi na tiba (111), uhandisi –umwagiliaji (7), ualimu (617), sayansi ya kilimo(20), uhandisi (70) na sayansi (98).

Taarifa iliyotolewa na Bodi ya Mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu (HESLB) kwenye tovuti ya bodi hiyo, imeonesha kuwa wanafunzi hao wamepewa siku 14 kufanya masahihisho hayo kuanzia Oktoba 24 hadi Novemba 6 mwaka huu.

HESLB imebainisha kuwa waombaji na wadhamini ambao hawakuweka saini zao kwenye fomu hizo, wanatakiwa kwenda wenyewe kwenye ofisi za bodi hiyo kwa ajili ya kufanya masahihisho hayo.

Pia kwa waombaji ambao hawakuambatanisha vyeti vya kuzaliwa, picha, nakala ya hati ya kusafiria au nakala za kadi za mpiga kura za wadhamini wao, wanaweza kutuma nyaraka hizo katika bodi wakiambatanisha na barua inayoonesha jina kamili la muombaji na namba ya cheti za kidato cha nne.

“Nyaraka zote zinatakiwa kuthibitishwa na Kamishna wa Viapo. Bodi inatoa tahadhari kwa waombaji kuwa makini na baadhi ya watu wasiowaaminifu ambao wanaweza kutumia nafasi hii kudai fedha.

“Ifahamike kuwa masahihisho yote yatafanyika nje ya mfumo wa mtandao (OLAS) kwani hakuna dosari inayohusu mfumo,” imeeleza sehemu ya taarifa hiyo.

HESLB itatafuta Sh bilioni 2 kutoka kwenye makusanyo ya wadeni au fedha za matumizi mengine, na Wizara itatoa Sh bilioni 1.1 ili kufikisha Sh bilioni 3.1 zitakazotumiwa na wanafunzi hao huku Serikali ikipanga kukopa vyuo ada ya wanafunzi hao.

Wakati wa udahili wa wanafunzi wa msimu wa masomo wa mwaka 2013 /2014 , bodi ilibaini maombi 6,364 yakiwa yamekosa taarifa muhimu za kuwafanya wapate mikopo.

Baadhi ya vitu vilivyokosekana katika fomu za waombaji ni kukosekana kwa saini ya mwombaji, cheti cha kuzaliwa, picha ya mdhamini, saini ya mdhamini, kukosekana saini ya mamlaka za Serikali za Mitaa na kukosekana kwa saini ya hakimu.

Hata hiyo, pamoja na bodi kutoa nafasi ya kurekebisha fomu kuanzia Agosti 16 hadi 30 mwaka huu, baadhi ya waombaji hawakuweza kusahihisha makosa yao kwa muda muafaka.

SOURCE:Habarileo

No tags for this post.

Leave a Reply

Switch to our mobile site