Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’ limepanga makundi ya fainali za mataifa ya Afrika kwa vijana chini ya umri wa miaka 17 Africa ‘2021 U-17 Cup of Nations’, zitakazounguruma nchini Morocco, baadae mwaka huu.

Tanzania ni miongoni mwa mataifa yaliyohusishwa kwenye upangaji huo wa makundi ikitokea ukanda wa Afrika Mashariki na kati sanjari na Uganda.

Timu ya taifa ya Tanzania chini ya umri wa miaka 17 ‘Serengeti Boys’ imepangwa Kundi B na timu za mataifa ya Nigeria, Algeria na Congo Brazaville.

Hii ni mara ya pili kwa Serengeti boys kupangwa kundi moja na Nigeria, kwani waliwahi kupatwa na mtihani kama huo kwenye Fainali za 2019 zilizofanyika jijini Dar es salaam.

Timu hizo zilifungua Fainali za mwaka huo Uwanja wa Benjamin Mkapa na wenyeji Tanzania walipoteza mchezo kwa kufungwa mabao 5-4, hivyo kukutana tena kwenye Fainali za mwaka huu itakua fursa kwa Serengeti Boys kulipa kisasi cha kufungwa nyumbani mwaka 2019.

Makundi mengine yaliyopangwa kwenye hafla iliyofanyika nchini Morocco leo jioni ‘KUNDI A’ lina timu za mataifa ya Uganda, Zambia, Ivory Coast na wenyeji Morocco.

‘KUNDI C’ lina timu za mataifa ya Cameroon, Senegal, Mali na Afrika Kusini.

Fainali za Mataifa ya Afrika chini ya umri wa miaka 17 kwa mwaka 2021 zimepangwa kuanza mwezi Julai.

Nzige wamtesa Waziri wa Kilimo
Kiongozi, Wachezaji Namungo FC kuondoka Angola