Rais wa Shirikisho la soka nchini (TFF), Jamal Malinzi kwa mara nyingine ametimiza ahadi yake kwa kuipeleka nje ya nchi timu ya taifa ya Tanzania ya vijana wenye umri wa chini ya miaka 17 ‘Serengeti Boys’ ambako itapiga kambi ya utulivu kabla ya kucheza na Congo-Brazzaville katika mechi ya mkondo wa kwanza kuwania nafasi ya kucheza fainali za Kombe la Mataifa ya Afrika kwa vijana wenye umri huo.

Benchi la ufundi lilimshauri Rais Malinzi kwamba kambi hiyo ipigwe jijini Victoria, kwenye Kisiwa cha Mahe nchini Shelisheli. Serengeti Boys inatarajiwa kuondoka nchini usiku wa kuamkia Jumatatu kwenda Shelisheli ambako itafanya mazoezi maalumu kwa ajili ya mchezo huo ambao utafanyika Septemba 18, 2016 kwenye Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam.

Hii ni mara ya pili kwa Malinzi kutimiza ahadi yake kwa wachezaji hao. Kwa mara ya kwanza aliahidi kuwapa kambi ya nje kama wangewatoa Shelisheli. Timu kweli ilikwenda Madagascar kabla ya kuivaa Afrika Kusini ‘Amajimbos’ na kuitoa na kwa sasa inakwenda Shelisheli kujipanga kwa ajili ya kuitoa Congo-Brazzaville.

Serengeti Boys ambayo ilipiga kambi Hosteli za TFF, zilizo Karume kwa siku nne kabla ya safari hiyo na Kocha Mkuu wa Serengeti Boys, Bakari Shime maarufu kama Mchawi Mweusi amesema kwamba anaamini kuwa mchezo ujao utakuwa mgumu kwa kuwa kila timu itajipanga kuvuka ili kucheza fainali hizo.

Rais Magufuli Atembelea Makaburi Ya Marais Watangulizi Wa Zanzibar Na Kusoma Dua Ya Pamoja
Kesi Ya Simba Na Yanga Kuhusu Kessy Yaahirishwa