Ujenzi wa Daraja la Salender litakalounganisha eneo la Coco Beach na eneo Agha Khan kupitia baharini Jijini Dar es Salaam unatarajiwa kuanza Mwezi Juni Mwakani baada ya Serikali ya Tanzania kukamilisha mchakato wa upatikanaji wa fedha za ujenzi kutoka benki ya Exim ya Korea.

Rais Magufuli amesema ujenzi wa daraja hilo litakalokuwa na urefu wa kilometa 7 zikiwemo kilometa 1.4 zitakazopita baharini, unatarajiwa kukamilika mwaka 2020 na daraja hilo litasaidia kupunguza adha ya msongamano wa magari katika Jiji la Dar es Salaam.

“Mchakato wa kulijenga hili daraja la Salender unaendelea vizuri kwa sababu hivi sasa kampuni ya Kikorea ambayo inafanya usanifu ipo kwenye hatua za mwisho na zabuni zinategemewa kutangazwa mwezi wa tatu Mwaka kesho na zitakwenda haraka, kwa hiyo mambo yakienda vizuri ujenzi unaweza kuanza mwezi wa sita, bahati nzuri fedha zote zipo na zimeshatolewa na Benki ya Exim ya Korea” Amesema Rais Magufuli.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amesema hayo leo tarehe 22 Septemba, 2016 muda mfupi baada ya kufanya Mazungumzo na Balozi wa Jamhuri ya Korea hapa nchini Mhe. Song Geum-Young, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Kwa upande wa, Balozi wa Korea hapa nchini Mhe. Song Geum-Young ametoa salamu za pole kufuatia maafa ya tetemeko la Ardhi yaliyotokea Mkoani Kagera na mikoa jirani, na ameahidi kuwa Korea itatuma timu ya wataalamu kuja kuona namna ya kusaidia.

Magufuli aipangua TTCL, amuondoa Mtendaji Mkuu na kumteua Kindamba
Waziri Mkuu apokea sh. Mil. 172.5 kwa ajili ya waathirika tetemeko Kagera