Jumla ya watu 28 wameuawa na wengine 30 kujeruhiwa kufuatia jaribio la uvamizi wa uporaji wa mifugo kaskazini mwa nchi Sudan Kusini.

Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo Afisa wa usalama wa eneo hilo Stephen Taker amesema
mauaji hayo yametokea siku mbili mfulizo kati ya Mei 16 na 17, 2022 katika Kaunti ya Leer Jimbo
la Unity nchini humo.

“Vijana wenye silaha walikuja na kushambulia eneo letu na watu wetu kumi ambao walikuwa
wakichunga Ng’ombe wamekufa ila kwa upande wao watu 18 walikufa na washambuliaji wengine
30 walijeruhiwa,” amefafanua Taker.

Kijana akichunga na Silaha

Amesema chanzo cha mauaji hayo kimetokana na Vijana wenye silaha kutoka kaunti jirani za
Mayendit na Koch kuvamia eneo hilo kwa minajili ya kuiba mifugo na kwamba upinzani uliotokea
ukasababisha vifo na majeruhi.

“Hii si mara ya kwanza kwa tabia hii kujitokeza hali hii imekuwa ikijirudia na matokeo yake
inaleta maafa kwa jamii na kuziacha baadhi ya kaya zikiwa na majonzi na visasi ni tabia ambayo
inapaswa kukomeshwa,” ameongeza Afisa usalama Taker.

Aidha Taker ameongeza kuwa Mwezi Februari mwaka huu pia watu wengine 72 waliuawa katika
eneo hilo kutoka na vita vya kikabila na kudai kuwa kaunti ya Leer imeathirika na mgogoro wa
kibinaadamu ambao ulizuka kutokana na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya mwaka 2013 na
2018.

“Kwanini isipatikane suluhu haya matatizo yanahitaji ufumbuzi na wala tatizo sio Ng’ombe ni
muendelezo wa visasi vya wakubwa na kwanini miaka yote hii bado watu hawa hawapati
muafaka,” amehoji Taker.

Kaunti ya Leer ni mojawapo ya maeneo yaliyoathiriwa na uvamizi nchini Sudan Kusini ambayo imekuwa ikikabiliwa na hali tete ya kisiasa, kiuchumi na kiusalama tangu ilipojinyakulia uhuru wake kutoka kwa Sudan mwaka 2011.

Eneo hili limekuwa mojawapo ya vitovu vya mzozo wa kibinadamu uliosababishwa na vita vya wenyewe kwa wenyewe kati ya Salva Kiir na Riek Machar vilivyosababisha karibu watu laki 4
kuuawa na mamilioni kuyakimbia makazi yao.

Hii inatokea baada ya miongo kadhaa ya vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyochochea
migawanyiko ya kikabila na mzozo wa kugombania mafuta na kufanya Sudan Kusini kuendelea kuwa na machafuko ya ndani yanayohatarisha usalama na kuvuruga maisha ya raia wake.

John Bocco akubali yaishe Ligi Kuu, vita yahamia ASFC
Azam FC: Tulistahili alama tatu dhidi ya Simba SC