Takribani watu 300 wamepotea na wanahofiwa kupoteza maisha baada ya kingo za bwawa la maji la kiwanda cha madini ya chuma kilichoko Kusini-Mashariki mwa Brazil kupasuka leo majira ya mchana.

Taarifa iliyotolewa na Serikali imeeleza kuwa kupasuka kwa bwawa hilo kumesababisha maji ya tope yenye kasi kubwa kusomba nyumba na watu kwenye mji wa Brumadinho, jimbo la Minas Gerais.

Ingawa bado idadi kamili ya watu waliopoteza maisha haijafahamika, miili ya wafanyakazi tisa wa kampuni hiyo waliokuwa wakipata chakula cha mchana imekutwa ikiwa imefunikwa na tope.

Kwa mujibu wa CNN, Gavana wa jimbo hilo, Romeu Zema amesema kuwa kuna uwezekano mdogo sana wa watu waliopotea kupatikana wakiwa hai.

Bado haijafahamika nini chanzo cha kubomoka kwa kingo za bwawa hilo linalomilikiwa na kampuni ya Vale ambayo ni kampuni kubwa zaidi ya madini nchini Brazil.

Tukio hilo limetokea ikiwa ni miaka mitatu tangu bwawa lingine la Kampuni ya Madini ya Minas Gerais iliyoko Mariana kubomoka na kusababisha vifo vya watu 19.

Ulaya wamtaka Maduro achague ‘kusuka au kunyoa’
Prof. Lipumba atangaza maombi