Chama cha wakunga Tanzania (TAMA) kimesema Tanzania ikabiliwa na upungufu wa wataalam wa afya ya uzazi hali inayopelekea 90% ya vifo vya uzazi kutokea hospitali hali ya kuwa hapo zamani vifo vilitokea majumbani kwa kukosa huduma stahiki za kitaalamu.

Kauli hiyo imetolewa na Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania Feddy Mwanga mbele ya waandishi wa Habari jijini Dar es Salaam katika mkutano ulioandaliwa na Shirika la Umoja wa Mataifa la Afya ya Uzazi na Idadi ya Watu Duniani UNFPA kuelekea maadhimisho ya siku ya wakunga Duniani.

Rais wa Chama cha Wakunga Tanzania Feddy Mwanga

Amesema kwa sasa Tanzania inakabiliwa na upungufu wa wafanyakazi wa afya kwa 48% na kuiomba serikali iajiri wafanyakazi wapya watakaosaidia kupunguza uhaba huo na kuongeza nguvu kazi katika huduma za afya ya mama na mtoto.

“Zamani ilikua wanawake wanakufa kwasababu wanajifungua mazingira hatarishi ila sasahivi wameacha kujifungua kwa njia za asili na wanaenda hospitali ila ndio wanakufa huko, Hii ni kutokana na system mbaya ya tiba kwa wazazi,” amesema Feddy.

Ameongeza kuwa 50% ya vifo vya wanawake wote Tanzania inatokana na kifafa cha uzazi na kutoka damu kabla na baada ya kujifungua.

Nae Meneja programu ya Afya ya mama na mtoto kutoka UNFPA Felister Mayalo Bwana amesema sababu zinazopelekea vifo vingi kutokea katika vituo vya afya ni Pamoja na kukosa ujuzi kamili wa ukunga, mazingira ya upatikanaji wa dawa, na wahudumu wengi hawatambui mda sahihi wa kutoa rufaa kwa mzazi.

Kwa upande wake Naibu Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA Tanzania, Dr. Wilfred Ochan katika salamu zake kwa washiriki wa mkutano huo amesema UNFPA ndilo shirika la Umoja wa Mataifa ambalo linajihusisha na masuala ya afya ya uzazi wakishirikiana na TAMA Pamoja na serikali ya Tanzania na hivyo kwa Pamoja katika maadhimisho ya siku ya wakunga duniani wanatakiwa kuangalia namna ya kuwapa uwezo wakunga ili kuendeleza juhudi za kupunguza vifo vya wazazi na Watoto wachanga.

Amesema UNFPA imekua ikisaidia wakunga katika nchi 120 Duniani kote kwa kuwa Wakunga ndio watu ambao wanatarajiwa kuwepo popote ambapo Mjamzito atakua anajifungua, biola kujali ni katika vita, katikati ya maambukizi ya magonjwa Mapya au nyakati zozote za shida.

Naibu Mwakilishi Mkaazi wa UNFPA Tanzania, Dr. Wilfred Ochan

Ameongeza kuwa kama Serikali zitawekeza katika kuwasaidia wakunga kila mwaka Duniani vifo milioni 4.3 vitaokolewa vya Watoto na wajawazito hadi kufikia mwaka 2035.

Kilele cha maadhimisho ya wakunga duniani ni tarehe 5 mei kila mwaka, na kwa mwaka huu maadhimisho hayo yatafanyika Jijini Dodoma.

Waziri Aweso awashika mkono mayatima
Rais Samia atangaza maombolezo siku 2