Waziri wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, William Lukuvi atakwenda katika Halmashauri ya Manispaa ya Tabora ili kutatua kero kubwa za ardhi.

Majaliwa amesema hayo wakati akizungumza na wananchi wa Manispaa hiyo katika mkutano wa hadhara uliofanyika kwenye Uwanja wa Chipukizi, baada ya wabunge na wananchi kueleza changamoto kubwa zinazowakabili ikiwe ya migogoro ya ardhi iliyodumu kwa muda mrefu.

“Waziri wa Ardhi atakuja hapa na ramani zake, atakutana na watendaji na kumaliza matatizo yote makubwa ya ardhi na yale madogo madogo yatashughulikiwa na Mkuu wa Wilaya,”.

Aidha, Majaliwa amesema wilaya zote zinatakiwa zihakikishe zinakuwa na shule moja ya kidato cha tano na sita kwenye kila tarafa nchini na Serikali itapeleka walimu.

Amesema uwepo wa shule hizo utaamsha ari ya wanafunzi kusoma kwa bidii, jambo litakaloongeza idadi ya wanaoendelea na masomo ya kidato cha tano na sita.

Pia, amewaagiza watendaji wote kuanzia ngazi ya halmashauri hadi vijiji wawasimamie wanafunzi wa kike na wahakikishe wanamaliza masomo bila ya kukatishwa.

“Huu ni mkakati wa Taifa tunataka watoto wa kike wote walindwe ili waweze kumaliza shule na marufuku kukatisha elimu yao, iwe kwa kuwapa ujauzito au kuwaoa, adhabu yake ni kali,”.

Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Agosti 20, 2018
Rais Magufuli afiwa na dada yake