Kampuni ya AAR Insurance Tanzania imezindua rasmi mfumo wa ‘smart health’ unaolenga kuboresha huduma kwa wateja na utendaji katika sekta hiyo.

Uzinduzi huo umefanyika leo Februari 11, 2021, jijini Dar es Salaam na kuhuhudhuriwa na mawakala wa bima na wadau wengine wa afya likitumika kutoa elimu zaidi kuhusu ufanisi na faida za mfumo huo ulioanzishwa mwaka 2020.

Akizungumza na vyombo vya habari wakati wa tukio hilo, Afisa Mkuu wa Operesheni (COO) wa AAR Insurance, Dkt. Emmanuel Bwana amesema kuwa kampuni hiyo imetumia maendeleo ya teknolojia kuhakikisha kuwa wateja wao wanapata huduma bora zaidi ya bima ya afya, kwa wakati na kwa urahisi.

“Hatua hii ni sehemu ya mchango wetu usiokoma kuunga mkono jitihada za serikali na wadau wengine katika kuhakikisha kila mmoja katika jamii anapata huduma bora ya bima ya afya,” amesema Bwana.

“Mfumo huu wa ‘smart health’ utawasaidia mawakala kutoa huduma kwa wakati na katika mazingira waliyopo wakiwa na mteja papo kwa papo. Kwahiyo, hakutakuwa na ulazima kwa wakala wa bima ya afya kupiga simu AAR ili aweze kupewa taarifa (quote),” ameongeza Bwana.

Mmoja kati ya washiriki wa mafunzo hayo, ambaye ni wakala wa bima ya afya ya AAR, Peter Sekidia ameipongeza kampuni hiyo akieleza kuwa mfumo huo utawasaidia kuongeza ufanisi katika kutoa huduma kwa wateja na kusema kuwa mfumo utaongeza kasi ya kupokea taarifa kutoka kwa mteja pamoja na kuwaongezea watoa huduma kasi ya kuthibitisha uhalali wa mteja.

Hatua ya Kampuni ya AAR Insurance kuanzisha mfumo wa smart health inaakisi jitihada za dunia katika kufanikisha kuwa na mfumo wa bima ya afya unaotolewa moja kwa moja kwa njia ya mtandao (eHealth System).

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Februari 12, 2021
Mahusiano Tanzania, Saudi Arabia yazidi kuchanua