Kampuni ya bima ya afya nchini ya AAR kwa kushirikiana na Jema Foundation inayojikita katika kutoa elimu kwa umma kuhusu ugonjwa wa saratani ya Mitoke ijulikanayo kama (Hodgkin’s Lymphomo), wametoa msaada kwa watoto wanaopata matibabu ya saratani katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili kwa kupitia kwa shirika lisilo la kiserikali la Tumaini La Maisha Tanzania, ambalo limejikita katika kusaidia matibabu ya watoto wenye saratani nchini kwa kushirikiana na Hospitali ya Taifa ya Muhimbili chini ya Wizara ya Afya.

Msaada uliowasilishwa ni pamoja na Chakula ikiwamo,Mchele,unga na sukari Pia wametoa vifaa tiba kama kipima joto cha kisasa (Digital Thermometer), sabuni maalum za kunawia na kuua bakteria (Hand Sanitizers), Kanga na mashine ya kukaushia nguo, mafuta ya kujipaka , sabuni za kuogea na kufulia, nepi za kisasa (diapers) na vingine.

Akizungumza baada ya kukabidhi msaada huo na kuwajulia hali watoto wenye tatizo la saratani, Msemaji wa AAR, Bi. Hamida Rashid amesema kuwa wanatambua juhudi zinazofanywa na serikali kusaidia watoto wenye saratani, hivyo wameamua kuunga mkono juhudi hizo.

“Kama bima ya afya inayoongoza na kutoa huduma bora, lengo la AAR ni kuhakikisha jamii inayotuzunguka inakuwa na afya bora. Tunatambua juhudi kubwa inayofanywa na Serikali,Hospitali ya Taifa ya Muhimbili na shirika la Tumaini La Maisha Tanzania katika kusaidia kupambana na saratani kwa watoto. Hivyo, tumeamua kuunga mkono juhudi hizi kwa vitendo kwa kusaidia sehemu ya mahitaji kwa watoto hawa. Kwetu sisi watoto ni sehemu muhimu ya moyo wa Taifa,” amesema Bi. Rashid.

Wafanyakazi wa Bima ya Afya ya AAR na Jema foundation wakiwa na watoto wanaopatiwa matibabu ya Saratani, katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili

Aidha, wawakilishi kutoka Bima ya afya ya AAR na Jema Foundation wametembelea Hosteli ya Ujasiri, wanapolelewa watoto wenye saratani wenye matibabu ya muda mrefu, Pia wametembelea wodi ya watoto wenye saratani ya Tumaini na Upendo katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Naye Afisa Mtendaji Mkuu wa Tumaini la Maisha Tanzania, Dkt. Patricia Scanlan amewashukuru AAR na Jema Foundation kwa msaada huo na kutoa wito kwa mashirika na watu binafsi kuiga mfano huo.

“Ninawashukuru sana AAR na Jema Foundation, ni hatua nzuri walioichukua. Saratani kwa watoto inamgusa kila mmoja kwenye jamii yetu. Tunapo wasaidia watoto hawa tunalisaidia Taifa zima” Amesema Dkt Scanlan

“Tunahudumia watoto zaidi ya 600 kwa mwaka wenye saratani hapa Muhimbili, wana mahitaji mengi. Jamii inapotuunga mkono kama hivi ni ishara ya ushindi katika kuokoa maisha ya watoto hawa,” aliongeza .

Dkt. Scanlan ametoa wito kwa jamii kuhakikisha inatoa kipaumbele kwa afya ya watoto kwa kuwapima saratani kwani wengi upoteza maisha kwa kuchelewa kupata matibabu husika kutokana na kutojua hali zao mapema.

Mahakama yabariki zuio la Trump kwa nchi za Kiislam kuingia Marekani
Ufisadi wagubika mazishi ya Mandela