Kampuni ya huduma za afya nchini, AAR Healthcare imepongezwa kwa kuwahudumia bure washiriki takribani 4,000 wa Kili Marathon iliyofanyika Jumapili iliyopita wilayani Moshi mkoani Kilimanjaro.

AAR Healthcare ilitoa huduma za uchunguzi wa afya za washiriki, huduma ya kwanza pamoja na huduma ya gari la wagonjwa (standby ambulance service).

Meneja wa Kampuni hiyo Mkoani Arusha, Dkt. Aggrey Mapunda aliwaambia waandishi wa habari kuwa kutokana na uzoefu wao katika ushiriki wa Kili Marathon, wamebaini kuwepo changamoto ya washiriki kutokuwa na elimu ya kutosha kuhusu umuhimu wa kufanya uchunguzi wa afya zao kabla ya kushiriki, suala ambalo alilielezea kuwa wamelifanyia kazi katika tukio la mwaka huu ili washiriki wawe na uhakika wa afya zao na hivyo kuepuka madhara hasi.

“Kitaalam, washiriki wote wa mbio wanapaswa kuchunguzwa afya zao, na sisi kama kampuni inayotoa huduma bora za afya tunaamini ni jukumu letu kutoa elimu inayohitajika pamoja na kuwapa huduma hiyo bure ili kuwahamasisha kuwa na utamaduni huo katika maisha yao ya kawaida,” alisema Dkt. Mapunda.

“Tunafahamu kuwa ajali na dharura za aina mbalimbali hutokea katika kipindi kama hiki, na hii ndio sababu imetufanya kutoa huduma ya gari la wagonjwa ambalo liko tayari muda wote kutoa huduma hapa, nalo pia tumelitoa bure,” aliongeza.

Aidha, Lydia Nasimiyu, mshiriki wa Kili Marathon kutoka Kenya ambaye ni mmoja kati ya waliofaidika na huduma ya afya bila malipo ya AAR aliizungumzia huduma hiyo na kuwapongeza kwa hatua waliyoichukua.

Wataalam wa afya wa AAR Healthcare wakitoa huduma kwa mshiriki wa Kili Marathon 2019

“Ningependa kuwashukuru AAR Healthcare kwa msaada wao wa huduma ya afya walionipa. Kweli nilipata huduma kwa muda. Ninashukuru wamekuwa hapa kuhakikisha washiriki tunapata huduma hii muhimu,” alisema Nasimiyu na kuongeza, “ningependa pia kuwapongeza kwa hiki walichokianzisha ili wengine pia waige kwa mafufaa ya wote na ninaamini huduma ya matibabu ni muhimu sana kwenye kila mashindano ya mbio (marathon).

 

Mbali na huduma hiyo, AAR Healthcare pia ni moja kati ya wadhamini wakuu wa Kili Marathon, na mwaka huu umekuwa mwaka wa pili kwao kudhamini tukio hilo.

“Tumekuwa tukifanya kazi na Kili-Marathon tangu mwaka jana kwa lengo la kufikisha kwa usahihi huduma bora za afya kwa watu. Na kwakuwa sisi ni wadau muhimu kwenye sekta ya afya na michezo, tunaamini kula vizuri na kwa usahihi pamoja na kufanya mazoezi ni kitu bora kwa afya ya kila mmoja wetu. Hivyo, tutaendelea kutoa mchango wetu na kuunga mkono kwa vitendo Kili Marathon kwa ajili ya kuhuisha afya bora,” alisema Meneja wa Maendeleo ya Biashara wa AAR Heathcare, Doscar Massaba.

Takribani watu 9,000 kutoka nchi mbalimbali walijiandikisha kushiriki kwenye Kili Marathn 2019, kwa mujibu wa tovuti ya waratibu wa mashindano hayo.

Kili Marathon imekuwa huhudhuriwa na watu wa nchi takribani 45 duniani kote na imekuwa chachu ya kuibua vipaji, kuchangia huduma za kijamii, kuongeza pato la nchi, kutangaza utalii na kuhamasisha mazoezi kwa afya bora ya jamii.

JPM atoa neno kuhusu tukio la kutekwa kwa Mo Dewji
Acacia kulipa fidia wananchi zaidi ya 200

Comments

comments