Mshambuliaji kutoka nchini Guinea Abdoul ‘Razza’ Camara ameshauriwa kuachana na soka, kufuatia matatizo ya moyo yanayoendelea kumakabili.

Mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 28 ambaye aliwahi kuitumikia klabu ya Derby County ya England msimu wa 2016–2017, amepewa ushauri huo na madakrati ambao wamekua akimshughulikia kimatibabu mara kwa mara.

Ushauri huo wa madaktari umekuja baada ya kutakiwa kufanya hivyo na viongozi wa klabu yake ya sasa Guingamp inayoshiriki ligi ya nchini Ufaransa, ambapo walimtaka apumzike kwa muda na ikiwezekana wavunje mkataba wake.

Hata hivyo Camara bado hajafanya maamuzi sahihi kufuatia ushauri huo wa kitabibu, ambao huenda ukamuokoa na janga la kupoteza maisha akiwa uwanjani, na badala yake bado anaonyesha dhamira ya kutaka kuendelea kupambana.

“Ninafikiria kwa kina jambo hii, ninataka kuendelea kucheza soka, kutokana na kuupenda sana mchezo huu, nimepokea ushauri wa madaktari lakini ninaendelea kuufanyia kazi,” Alisema mshambuliaji huyo alipohojiwa na mwandishi wa habari wa tovuti ya footmercato.

“Hii ni mara ya pili ninashauri kuachana na soka, viongozi wa klabu nao waliwahi kuniambia jambo hilo, lakini kwa muda sasa ninaendelea kujifikiria, suala kubwa hapa ni hofu ya kupoteza maisha nikiwa uwanjani, ”

“Nitasubiri kwa muda wa majuma matatu ili kutazama maendeleo ya hali yangu, na baada ya hapo nitatoa maamuzi sahihi.

“Tangu nikiwa na umri wa miaka 13, maisha yangu yamekua katika mchezo wa soka. Nilijitahidi kwa hali zote ili nifanikishe lengo la kuwa mchezaji mkubwa duniani, na jambo hilo ndilo linanipa wakati mgumu wa kufanya maamuzi ya kuachana na mchezo huu.”

“Wakati mwingine najihisi kama nimeingiwa na shetani, lakini uhalisia wa mambo huwa naupata kutoka kwa madaktari ambao mara kadhaa wamekua wakinishauri kuhusu tatizo langu ya moyo.”

Camara alipokua nchini England alifanikiwa kucheza michezo 26 akiwa na klabu ya Derby, na alifunga katika mchezo wa mzunguuko wa nne wa kombe la FA dhidi ya Leicester City mwaka 2017.

Mbali na klabu hiyo ya England na Guingamp, Camara pia amewahi kuzitumikia klabu nyingine za Ufaransa Rennes na Sochaux, PAOK ya Ugiriki na Real Mallorca ya Hispania.

Camara alianza kucheza soka la kulipwa nchini Ufaransa, na tayari ameshazitumikia timu za taifa hilo chini ya umri wa miaka 17, 18 na 21, na baadae aliamua kuthibitisha kuitumikia timu ya taifa ya Guinea. Katika timu hiyo Camara amecheza michezo 16 na kufunga mabao manne.

Serikali kuongeza fedha za TASAF
TCRA yataka wateja wa DSTV, AZAM na ZUKU waliolipishwa kuwasilisha taarifa zao