Serikali imewataka abiria wanaosafiri mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi kuchukua tahadhari juu ya maambukizi ya UVIKO -19 huku wakiaswa kupaza sauti zao pindi wanapoona uvunjifu wa sheria za usalama barabarani ili kuepusha ajali zinazosababisha vifo na majeruhi.

Hayo yamesemwa na Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi ambae pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Usalama Barabarani, Khamis Hamza Chilo alipofanya ziara, alfajiri ya kuamkia leo Agosti 29, lengo ikiwa kutoa tahadhari kwa wadau wa vyombo vya usafiri juu ya tahadhari ya ajali wawapo barabarani sambamba na kujikinga na maambukizi ya UVIKO-19 kwa abiria hao.

Akizungumzia madereva wanaoenda mwendokasi bila kufuata sheria za usalama barabarani Naibu Waziri Chilo amesema tayari serikali imeanza utaratibu wa kuchukua leseni ya udereva kwa dereva yoyote atakaethibitika kusababisha ajali kwa uzembe wake.

“Hivi karibu mmeona jinsi dereva wa basi la Sauli linalofanya safari zake kati ya Dar es Salaam na Tunduma alivyoyapita magari mengine bila kuchukua tahadhari sasa ile ni hatari, ametokea Mbeya mbali kweli anakuja kupata ajali Kibaha alikuwa na haraka gani? tayari serikali kupitia mamlaka husika ikiongozwa na Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani nchini, Wilbrod Mutafungwa tushachukua leseni yake na tumemfungia kwa muda wa miezi sita na sasa atarudi darasani akajifunze upya udereva, kwenye kulinda maisha ya wananchi hatutaki mchezo,” Amesema Naibu Waziri Chilo

Akizungumza kwa niaba ya madereva wengine, Dereva wa Basi la Al Saedy, Alex Emmanuel ameomba elimu itolewe kwa madereva wa malori kwani ndio wamekua chanzo cha ajali nyingi za barabarani hali inayopelekea kutokukoma kwa matukio ya ajali huku Mkuu wa Kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Dodoma, Mratibu Mwandamizi wa Polisi, Boniface Mbao akiweka wazi kuwepo kwa utaratibu wa utolewaji wa elimu na ukaguzi wa mabasi kabla ya kuanza safari na basi linalokutwa na hitilafu basi huzuiwa lisiondoke.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Augusti 30, 2021
Namna bora kuboresha makalio kwa wanawake