Mabingwa wa soka nchini England, Chelesea wapo katika mbio za kumsaka kiungo kutoka nchini Ujerumani na klabu ya Real Madrid ya nchini Hispania, Toni Kroos.

Chelsea wamelijumuisha jina la kiungo huyo katika orodha ya wachezaji ambao wanawapa kipaumbele cha kuwasajili wakati wa majira ya kiangazi kutokana na kuamini ataweza kuhimili mikiki mikiki ya klabu hiyo kuelekea msimu ujao wa ligi ya nchini England ambao unatarajiwa kuwa na upinzani wa hali ya juu.

Toviti ya habari ya Calciomercato ya nchini Italia, imedai kuwa Kroos mwenye umri wa miaka 25, ameingia kwenye rada za Chelsea ambayo inahaha kusuka kikosi chake upya baada ya kupoteza mwelekeo msimu huu.

Mmiliki wa The Blues, Roman Abramovich anapanga kutumia kiasi kikubwa cha fedha kuirudisha klabu yake katika mwelekeo sahihi, baada ya kuonekana dhahiri kimefeli kutetea taji lake la Premier League msimu huu.

Hata hivyo huenda Chelsea wakapata wakati mgumu wa kuhimili ada ya usajili wa Kroos ambayo inakadiriwa kufikia pauni million 234, ili ikidhi mahitaji ya mkataba wake kwa mujibu wa mtandao wa Football Leaks.

Kroos aliyejiunga na klabu ya Real Madrid mwaka 2014 akitokea FC Bayern Munich, ana mkataba wa kuendelea kubaki Santiago Bernabeu hadi mwaka 2020, lakini Abramovich anaweza kuonyesha ‘jeuri ya fedha’ na kumng’oa kiungo huyo ambaye aling’aa akiwa na mabingwa wa soka duniani timu ya taifa ya Ujerumani kwenye fainali za kombe la dunia kule nchini Brazil.

Ezequiel Lavezzi Kulipwa Mara Mbili Na Nusu Kwa Juma
FC Bayern Munich Wamgeuzia Kibao Pep Guardiola