Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa (TAKUKURU) mkoa wa Njombe, imemfikisha katika mahakama ya hakimu mfawidhi wilaya ya Makete, Honorata Mwinuka katibu muhtasi halmashauri ya wilaya ya Makete na kumfungulia kesi na CC.11/2019 kwa makosa ya kughushi vyeti vya taaluma chini ya sheria ya kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake kaimu mkuu wa Takukuru mkoa wa Njombe, Charles Mulebya amesema kuwa mshtakiwa kwa lengo la kujipatia ajira kama katibu muhtasi alighushi vyeti vya taaluma akionyesha kuwa alisoma kozi ya ukatibu muhtasi katika chuo cha utumishi wa umma (TPSC) Dar es salaam.

Ambapo alihitimu na kupewa cheti cha kumaliza kozi hiyo na kile cha matokeo huku akijua hajawahi kujiunga na chuo hicho wala kuhitimu kozi ya ukatibu muhtasi.

Aidha, Mulebya amesema kuwa kitendo cha mshtakiwa kughushi vyeti ni kinyume na K/F cha 333,335(a)337 na 342 vyote vya sheria ya kanuni ya adhabu kama ilivyofanyiwa marekebisho mwaka 2002.

Hata hivyo, amesema kuwa kesi dhidi ya mshtakiwa ipo mbele ya hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Makete, Jonathan Mpitanjia.

Makamu wa Rais azindua mbio za Mwenge wa Uhuru 2019
Katibu wa hamasa na Chipukizi ahamasisha elimu mkoani Njombe