Mshambuliaji Super Mario Balotelli huenda akarejesa mjini Milan nchini Italia, kujiunga na klabu ya AC Milan ambayo ilikubali kumuuza mwanzoni mwa msimu uliopita kwenye klabu ya Liverpool kwa paund million 16.

AC Milan, wameonyesha kuwa tayari kumsajili kwa mkopo mshambuliaji huyo ambaye kwa sasa hana nafasi katika kikosi cha kwanza cha Liverpool ambacho katika safu ya mashambilizi kinaongozwa na Christian Benteke.

Taarifa kutoka mjini Milan zimeeleza kwamba, viongozi wa AC Milan wamekua na vikao vya mara kwa mara ambavyo vimebeba dhumuni la usajili wa Balotelli.

Mtendaji mkuu wa AC Milan, Adriano Galliani, mwishoni mwa juma lililopita alithibitisha kufanyika kwa vikao hivyo na kusema kwa pamoja wamekubaliana kumrejesha Balotelli kwa mkopo.

Hata hivyo Galliani ametoa angalizo kwa Balotelli kwa kumtaka awe makini na fadhila wanayotaka kumuonyesha katika kipindi hiki, ambacho imeonekana kipaji chake kipo hatarini kuteketea kutokana na kutocheza mara kwa mara.

Kiongozi huyo amesema Balotelli atapewa nafasi ya mwisho kuthibitisha uwezo wake wa kisoka, na awe tayari kuachana na mamabo ya kipuuzi ambayo yamekua yakiwakera viongozi pamoja na watu wanaomzunguuka.

Galliani amesisitiza kuwa, endapo Balotelli atafikia lengo analolikusudia, huenda wakamsajili moja kwa moja mara tu mkataba wake wa mkopo akitokea Liverpool utakapomalizika.

AC Milan hii leo wanatarajia kutuma ofa ya kumsajili mshambuliaji huyo mwenye umri wa miaka 25 kwa mkopo, na kama mambo yatakuwa mazuri huenda kesho akafanyiwa vipimo vya afya huko mjini Milan.

Kabla ya AC Milan kuthibitisha mpango wa kumrejesha Balotelli nchini Italia kwa mkopo, klabu ya Sampdoria ilionyesha nia ya kumsajili moja kwa moja mshambuliaji huyo, lakini aligoma na kusisitiza suala la kuhitaji kwenda nchini Hispania.

Mourinho Aipotezea Adhabu Ya John Terry
Chadema Yadai Kumepata Kadi Feki Za NEC Kuipa Ushindi CCM, Ni Mamilioni