Klabu ya AC Milan ya Italia imeonyesha nia sahihi ya kutaka kumsajili beki wa kati kutoka nchini Ivory Coast na klabu ya Manchester United Eric Bailly, kupitia dirisha dogo la usajili, ambalo litafunguliwa rasmi mwezi Januari 2019.

Kwa mujibu wa taarifa zilizochapishwa kwenye tovuti ya Tuttosport, AC Milan wamethibitisha kuwa tayari kuanza mazungumzo na uongozi wa Man Utd kuhusu usajili wa beki huyo, ambaye kwa sasa hana nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Jose Mourinho.

Uongozi wa klabu hiyo ya mjini Milan unaamini usajili wa beki huyo mwenye umri wa miaka 24, huenda ukawa suluhisho kwenye kikosi chao, ambacho kwa sasa hakifanyi vizuri katika michuano ya ligi ya Serie A, pamoja na Europa League.

Hata hivyo mpaka sasa uongozi wa Man Utd haujatoa taarifa zozote kuhusu ukweli wa kumuweka sokoni Bailly itakapofika mwezi Januari, japo kila kukicha taarifa za beki huyo kuhitajika katika klabu kadhaa za barani Ulaya zinaendelea kutolewa kwenye vyombo vya habari.

Mbali na AC Milan ya Italia, klabu za Uingereza kama Arsenal, Tottenham na Chelsea zinatajwa kumuwania beki huyo, aliyesajiliwa na Man Utd mwaka 2016 akitokea Villareal ya Hispania.

Kwa mara ya mwisho Bailly alionekana akicheza kwenye kikosi cha kwanza cha Man Utd, wakati wa  mchezo wa ligi kuu dhidi ya Newcastle United uliochezwa Oktoba 06.

Hata hivyo katika mchezo huo uliomalizika kwa Man Utd kuibuka na ushindi wa mabao matatu kwa mawili, Bailly alicheza kwa dakika 19 pekee, kabla ya kutolewa na nafasi yake kuchukuliwa na mchezaji mwingine.

Kalemani avunja Bodi ya Wakurugenzi ya Wakala wa Nishati Vijijini (REA)
Video: Hakuna aliyesalama, Polisi yaonyesha alipofichwa Mo Dewji