Aliyekua meneja wa klabu ya Man City, Manuel Pellegrini ameripotiwa kuwa katika hatua za mwisho za kukamilisha mpango wa ajira katika klabu kongwe mjini Milan nchini Italia, AC Milan.

Taarifa kutoka nchini humo zinaeleza kwamba, meneja huyo kutoka nchini Chile, amekuwepo mjini Milan kwa siku kadhaa na wakati wowote kuanzia hii leo atakamilisha mpango wa kusaini mikataba kabla ya kutangazwa rasmi kuwa mkuu wa benchi la ufundi la AC Milan.

Hatua za mazungumzo baina ya pande hizo mbili, zilifanywa kimya kimya kabla ya vyombo vya habari nchini Italia kushtukia jambo hilo usiku wa kuamkia hii leo.

AC Milan walitangaza kumtimua aliyekua meneja wa kikosi chao Siniša Mihajlović, Aprili 12 mwaka huu na walimteua kocha wa timu ya vijana Cristian Brocchi kuwa meneja wa muda hadi mwishoni mwa msimu wa 2015-16.

Mipango ya kuchukuliwa kwa Pellegrini, inadhihirisha wazi AC Milan wamepania kufanya vyema kwa kutumia nafasi ya meneja huyo kuwa huru katika kipindi hiki, baada ya kuachana na Man City ambao watakuwa na meneja mpya (Pep Guardiola) kuanzia msimu wa 2016-17.

Pellegrini alidumu kwa kipindi cha miaka mitatu, akiwa na Man City ya nchini England (2013–2016) na alifanikiwa kutwaa mataji matatu likiwemo taji la ligi kuu ya soka nchini humo, kombe la FA pamoja na kombe la ligi (Capital One Cup).

Kabla ya kuelekea Etihad Stadium, Pellgrini alikua nchini Hispania akifanya kazi zake za umeneja kwenye klabu ya Malaga CF kuanzia mwaka 2010–2013, na kabla ya hapo alikua meneja wa mabingwa wa soka barani Ulaya Real Madrid (2009–2010).

Akiwa Estadio Stantiago Bernabeu, Pellegrini alifanikiwa kuwasajili wachezaji kama Cristiano Ronaldo, Kaka, Karim Benzema pamoja na Xabi Alonso.

Meneja huyo alianza shughuli zake za umeneja nchini Hispania mwaka 2004 akiwa na klabu ya Villarreal ambayo akliitumikia hadi mwaka 2009.

Klabu nyingine alizowahi kuzitumikia kama meneja ni Universidad de Chile (1988–1989), Palestino (1990), Palestino (1991–1992),         O’Higgins (1992–1993), Universidad Católica (1993–1995), Palestino (1998), LDU Quito (1998–2001), San Lorenzo (2001–2002) pamoja na River Plate (2002–2003)

Simba Yafanikiwa Kwa Jamal Simba Mnyate
Hans Poppe: Kamati Yangu Haipendekezi Mchezaji Wa Kusajiliwa