Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola ameitaka jamii ya kitanzania hususani waandishi wa habari kuacha kufuatilia tukio la kupotea mbwa wa Jeshi la Polisi anayejulikana kwa jina la Hobby, kwa kuwa jambo hilo kwa sasa lipo chini ya uchunguzi.

Waziri Lugola ametoa kauli hiyo leo Julai 21, 2018 wakati alipokuwa anazungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam mara baada ya kumaliza ziara yake katika vyombo vya Ulinzi ambavyo vipo chini ya Wizara  yake na kubaini changamoto na madudu mbalimbali yaliyokuwa yakifanywa na askari hao kwenye maeneo yao ya kazi.

“Nimekubaliana na Ispekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro jana Julai 20, 2018 kwamba waingie kwa undani sana kufanya uchunguzi wa nini kimetokea kwenye kikosi hicho halafu baadae wanipe taarifa. Kwa hiyo jambo hili sasa linaenda kufanyiwa kazi na Inspekta Jenerali wa Polisi”,amesema Waziri Lugola.

Pamoja na hayo, Waziri Lugola ameendelea kwa kusema “na nyinyi wanahabari kwa kuwa jambo hili linaenda kufanyiwa uchunguzi naomba sasa tuache kufuatilia jambo hili ili chombo husika kiweze kuchunguza halafu tuone nini cha kufanya”.

Julai 19, 2018, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola alibaini upotevu wa mbwa huyo wakati alipokuwa kwenye ziara yake katika Kikosi cha Farasi na Mbwa kilichopo eneo la Bandari Jijini Dar es Salaam na kumuagiza IGP Sirro kutoa maelezo ya upotevu wa mbwa.

Mbali na hilo, Waziri wa Mambo ya Ndani, Kangi Lugola amewaonya wananchi kuacha tabia ya kupotosha taarifa na matamko yake ambayo anayatoa kwenda sehemu husika.

Habari kubwa katika Magazeti ya Tanzania leo Julai 22, 2018
Picha: Rais Magufuli akitoa salamu za pole familia ya Kikwete