Chama cha ACT-Wazalendo, kimehoji kuhusu taarifa ya matumizi ya zaidi ya shilingi bilioni 5 za msaada kwa waathirika wa tetemeko la ardhi, iliyotolewa na Mkuu wa Mkoa wa Kagera, Meja Jenerali mstaafu, Salumu Kijuu.

Juzi, Mkuu huyo wa Mkoa wa Kagera alieleza kuwa fedha zote zilizotolewa (sh bilioni 5.428) zitatumika katika kukarabati miundombinu ya serikali pamoja na sehemu za umma zinazotoa huduma muhimu huku akiwataka wananchi kutosubiri bali waanze kuzikarabati nyumba zao wenyewe.

“Natoa wito kwa wananchi walioathiriwa na tetemeko la ardhi ambao hawajaanza kukarabati nyumba zao, waige wale wanaorejesha miundombinu wao wenyewe. Serikali itaendelea kusaidia makundi maalum,” alisema Mkuu huyo wa Mkoa.

Akizungumzia kauli hiyo, Katibu wa Kamati ya Maendeleo ya Jamii ya chama cha ACT-Wazalendo, Janeth Rithe aliipinga kauli hiyo na kutaka Serikali kutafakari upya na kuwapa kipaumbele zaidi wananchi walioathirika.

Alisema kuwa ingekuwa busara zaidi kwa Serikali kufahamu kuwa katika kushughulikia maafa, hatua ya kwanza ingekuwa kurudisha hali ya maisha ya watu na sio kukarabati miundombinu kwanza.

“ACT-Wazalendo tunaiomba Serikali kuelekeza misaada iliyopatikana kwa wananchi walioathirika ili waweze kurudi katika maisha yao ya kawaida ikiwemo kuwasaidia kukarabati na kuwajengea nyumba za kuishi,” Rithe anakaririwa.

Tetemeko la ardhi liliikumba mikoa ya kanda ya ziwa Septemba 10 mwaka huu na kupelekea maafa na uharibifu wa makazi na miundombinu. Watu 17 waliripotiwa kufa na 560 wakijeruhiwa. Zaidi ya nyumba 2000 zilibomoka kabisa.

Alexis Sanchez Kuiongoza Chile Dhidi Ya Uruguay
Trump apiga teke bakuli la ‘mshahara wa Urais’