Chama cha ACT-Wazalendo kimetangaza kufanya Mkutano Mkuu wa ‘Kidemokrasia’ Oktoba 8 mwaka huu katika ukumbi wa Makumbusho ya Taifa jijini Dar es Salaam, kuanzia saa tatu asubuhi hadi jioni.

Kwa mujibu wa taarifa rasmi ya mkutano huo iliyotolewa na uongozi wa chama hicho, utawajumuisha wananchi wote pamoja na viongozi wa chama hicho tofauti na mikutano mikuu ya kawaida.

“Tofauti na Mkutano Mkuu wa kawaida ambao huusisha wajumbe mahsusi, Mkutano Mkuu wa Kidemokrasia unatoa fursa kwa wanachama na wananchi wa kawaida kushiriki na kuhoji mambo mbalimbali yanayohusu Chama cha ACT Wazalendo, nchi ya Tanzania na bara la Afrika. ACT Wazalendo ndicho chama pekee kinachotoa fursa ya namna hii kwa wanachama na wananchi,” imeeleza taarifa hiyo.

Chama hicho kimeitisha mkutano mkuu huo kwa staili ya kipekee huku bado kukiwa na marufuku ya polisi kwa mikutano ya hadhara na huenda mkutano huo pia ukakumbwa na kile kilichoukumba mkutano wa ndani wa mjumbe wa halmashauri kuu ya Chadema, Edward Lowassa alipokuwa mjini Bukoba mwezi uliopita. Jeshi la polisi lilizuia kufanyika kwa mkutano huo wa ndani kutokana na kuhudhuriwa na wananchi wengi tofauti na ilivyo kwa mikutano ya ndani ya kawaida.

Hivi karibuni, Jeshi la polisi liliruhusu kufanyika kwa mikutano ya ndani huku likiendelea na marufuku ya mikutano ya hadhara.

ACT-Wazalendo wameeleza kuwa, pamoja na mambo mengine, Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe atawasilisha mada kuhusu hali ya kisiasa nchini pamoja na michakato ya katiba barani Afrika.

“Kupitia Mkutano huu, Kiongozi wa Chama atawasilisha uchambuzi mpana na wa kina zaidi kuhusu hali ya nchi yetu kiuchumi, kisiasa na kijamii tangu Serikali ya Awamu ya Tano iingie madarakani,” imeeleza.

Wengine wanaotarajiwa kuwasilisha mada kuhusu hali ya nchi ni pamoja na Mwenyekiti wa chama hicho, Mama Anna Mghwira, Mshauri wa Chama Prof. Kitila Mkumbo na Meya wa Manispaa ya Kigoma-Ujiji Hussein Ruhava.

Chama hicho kimeeleza kuwa mbali na wananchi wote kwa ujumla, kimetuma mualiko rasmi kwa vyama vyote vya siasa nchini pamoja na asasi za kiraia.

Video Mpya: Barakah Da Prince feat. Ali Kiba - Nisamehe
Mahusiano: Mitandao chanzo cha wanawake kupenda mapenzi ya gizani 18+