Chama cha ACT-Wazalendo, kimejibu mapigo saa chache baada ya Msemaji wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Christopher Ole Sendeka kuvikosoa vikali vyama vya upinzani nchini kikiwemo chama hicho.

Ole Sendeka aliivaa ACT-Wazalendo na viongozi wa vyama vingine vya siasa akiwemo Mjumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Edward Lowassa akiwataka waache upotoshaji kuhusu utendaji wa Serikali ya Awamu ya Tano.

ACT-Wazalendo wamemtaka Ole Sendeka kuachana na kile walichokiita porojo na badala yake ajikite katika kuishauri Serikali ya CCM kutekeleza ahadi zake kwa wananchi.

“Sasa ni mwaka mmoja tangu wachaguliwe, lakini hakuna madawa hospitalin, hakuna mikopo kwa Wanafunzi wa Elimu ya Juu, hakuna ajira mpya. Hakuna kupanda mishahara kwa #WatumishiWaUmma, hakuna hata jiwe la msingi la Kiwanda kipya lililowekwa tokea ya awamu ya tano iapishwe,” chama hicho kimeandika kupitia Twitter.

Katika hatua nyingine, Katibu wa Bunge na Serikali za Mitaa wa chama hicho, Habibu Mchange wakati akizungumza na wanahabari jana jijini Dar es Salaam alijibu hoja ya Ole Sendeka kuhusu uchunguzi wa mali za  viongozi wa Kamati za Bunge akiwemo Kiongozi Mkuu wa chama hicho, Zitto Kabwe.

Mchange alisema kuwa chama hicho kinaitaka Serikali kuanza uchunguzi mara moja dhidi ya Kabwe ili kujiridhisha.

“Tunavitaka vyombo vya uchunguzi vianze kazi hiyo mara moja, kwani tunaamini kuwa kama kuna kiongozi ambaye mali, madeni, maslahi na akaunti zake ziko wazi basi ni ndugu Zitto,” alisema Mchange.

Akizungumzia hoja ya Ole Sendeka kutaka Wenyeviti wa Kamati za Bunge kuchunguzwa na kumhusisha Kabwe na ufisadi wa shilingi milioni 800 za ardhi ya NSSF, alisema kuwa hakuna ripoti ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) inayomhusisha mwanasiasa huyo na sakata hilo.

Mchange alisema chama chake kina taarifa ya CAG ambayo inaonesha alitoa hati safi kwa NSSF kwa hesabu za Mwaka wa Fedha 2014/15 na kuainisha kuwa hakukuwa na ufisadi wa aina yoyote.

Sumaye adai amepata taarifa ya kutimuliwa nyumbani kwake pia
Video: DC Mjema atoa agizo kwa wafanyabiashara Ilala