Msajili wa Vyama vya Siasa, Jaji Francis Mutungi ametishia kukifutia usajili Chama cha ACT-Wazalendo, kutokana na kukiuka Sheria ya Vyama vya Siasa ikiwamo kuchoma moto bendera ya Chama cha Wananchi (CUF)

Jaji Mutungi ametoa siku 14 kwa chama hicho kuwasilisha maelezo ya maandishi kuwa ni kwanini usajili wake wa kudumu usifutwe kutokana na kukosa sifa kwa kukiuka Sheria za Vyama vya Siasa na kutowasilisha ripoti ya ukaguzi kuanzia mwaka 2013-17.

Taarifa iliyotolewa na Msajili wa Vyama vya Siasa, imesema kuwa kutowasilisha ripoti ya ukaguzi ya mwaka wa fedha 2013/14, chama hicho kinakuwa bado hakijakidhi matakwa ya Msajili wa Vyama vya Siasa na hivyo chama hicho pia kinakuwa kimekiuka Sheria ya Vyama vya Siasa Sura ya 258.

Aidha, baada ya Mahakama Kuu kutoa uamuzi wa kesi Na. 23 ya mwaka 2016, iliyokuwa inahoji uhalali wa Profesa Ibrahimu Lipumba, Machi 18, 2019, kumekuwa na matukio ya uvunjifu wa sheria ikiwemo kuchoma moto bendera za CUF, uliofanya na watu wanaoaminika kuwa ni wafuasi wa aliyekuwa Katibu Mkuu wa CUF, Maalim Seif, wanaodai sasa ni wanachama wa ACT- Wazalendo. Kitendo cha kuchoma bendera ya chama cha siasa ni kukiuka kifungu cha 11C, cha sheria ya vyama vya siasa.

“Vile vile katika mitandao ya kijamii imeonekana video watu wakipandisha bendera ya ACT kwa kutumia tamko takatifu la dini ya kiislamu (Takbir), kitendo hiki pia ni kukiuka kifungu cha (9) (1) (c) cha Sheria ya Vyama vya Siasa inayokataza kuwa na ubaguzi wa kidini kwa wanachama wake na kifungu cha (9) (2) (a), kinachokataza katiba, sera au vitendo vya chama cha siasa kuhamasisha au kueneza dini fulani,” imesema taarifa hiyo ya msajili.

Hata hivyo, pamoja na mambo mengine, msajili amekumbushia onyo lake la Machi 18 mwaka huu akikemea kitendo cha wananchi wa chama hicho huku akionyesha mshangao kwa chama hicho kutochukua hatua ya kukemea suala hilo akisema chama hicho kimeafiki au kilitoa maelekezo kufanyika kwa vitendo hivyo.

 

 

Ndugai atua Zanzibar, ‘Hakikisheni 2020 tunabaki madarakani’
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Machi 26, 2019

Comments

comments