Meneja aliyeiwezesha klabu ya Sevilla kutwaa ubingwa wa Europa League mara tatu mfululizo, Unai Emery anatazamia kubadili mazingira ya kazi yake kwa kuachana na soka la nchini Hispania na kujaribu bahati yake huko nchini England.

Emery, anatajwa kuwa katika mipango mizuri ya kukaribia kupata ajira jijini Liverpool katika klabu ya Everton, ambayo kwa sasa haina meneja kufutia kutimuliwa kwa Roberto Martinez majuma mawili yaliyopita.

Everton, wanampa nafasi kubwa Emery kuwa mkuu wao wa benchi la ufundi, kwa kuamini anafaa kuwa sehemu ya watu watakaowezesha mpango wa kufikia malengo ya kufanya vyema msimu ujao wa ligi.

Hata hivyo meneja huyo kutoka nchini Hispania, hajawahi kuzungumza suala lolote kuhusu mpango wa kutakiwa na klabu ya Everton, ambayo ina upinzani mkubwa na Liverpool ambayo alifanikisha harakati za kuibamiza katikati mwa juma lililopita, kwenye mchezo wa hatua ya fainali ya Europa League.

Emery mwenye umri wa miaka 44, aliwahi kuhusishwa na mipango ya kutaka kujiunga na moja ya klabu za Newcastle Utd na Aston Villa zote za nchini England, wakati zikihitaji usaidizi wa mbadala wa wakuu wa mabenchi ya ufundi.

Wakati huo huo, uongozi wa klabu ya Everton, umeliorodhesha jina la meneja wa klabu ya Southampton, Ronald Koeman katika harakati za kumsaka mbadala wa Martinez, lakini Emery bado anatajwa kuwa chaguo la kwanza kwa viongozi walio wengi huko Goodson Park.

Magwiji Wa London Wapigana Vikumbo
David Moyes Kurejea Katika Soka La England?

Comments

comments