Mzee mmoja aliyetambulika kwa jina la Visu Urembo (80) amefariki dunia baada ya kuchomwa mkuki sehemu ya ubavuni mwa mwili wake, katika mgogoro wa wakulima na wafugaji uliotokea Lukenge, Tarafa ya Ruvu, Kibaha Vijijini mkoani Pwani.
 
Kamanda wa Polisi mkoa wa Pwani, ACP Wankyo Nyigesa amethibitisha kutokea kwa tukio hilo, ambapo amesema tukio hilo limetokea machi 26 mwaka huu baada ya kutokea tafrani kati ya wakulima na wafugaji.
 
Amesema kuwa mzee Urembo kabla ya kufikwa na umauti alikimbizwa kituo cha afya Mlandizi, ambapo baadaye alikimbizwa katika hospital ya Tumbi kwa matibabu zaidi lakini kabla ya kupatiwa matibabu madaktari waligundua kuwa tayari ameshafariki.
 
Aidha, Wankyo amesema kuwa wafugaji hao waliingiza mifugo yao (Ng’ombe) kwenye bwawa linalotumika katika shughuli za kibinadamu ikiwemo kunywa, kufulia, kupikia, kwa kuona hivyo wakulima walienda na mihemko kuwazuia wafugaji hao, ndipo wafugaji hao walipoanza kurusha mikuki na vitu vyenye ncha kali na kusababisha kifo cha mzee huyo na wengine watatu kujeruhiwa vibaya.
 
“Polisi tulifika eneo la tukio alfajiri Machi 27 mwaka huu ,na kutuliza tafrani hiyo na sasa hali ni shwarii,”amesema kamanda Wankyo
 
Hata hivyo, amewataja waliojeruhiwa kuwa ni pamoja na John Kisukari Urembo (50) ambaye ni mwenyekiti wa serikali ya kijiji cha Lukenge. Maximilian Evarist (34) mtendaji wa kijiji cha Lukenge na Adam Onesha ambaye ni mwenyekiti wa kamati ya maji kijijini hapo .
 
Kwa upande wake, mkuu wa wilaya ya Kibaha Assumpter Mshama ameyataka makundi hayo yaheshimiane na kujenga upendo badala ya kujiona kundi moja ni zaidi ya kundi jingine.

Video: Ridhiwani Kikwete akabidhi mradi wa maji safi na salama
Polisi kigoma yakamata bunduki za kivita, risasi 125