Afisa wa Benchi la Ufundi wa Mabingwa wa Soka nchini Sudan Al Hilal ‘Omdurman’ Nabil Kouki, amekiri kuitamani Young Africans katika mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki.

Kikosi cha Al Hilal kimeweka kambi jijini Dar es salaam-Tanzania, kwa ajili ya kujiandaa na mchezo wa Ligi ya Mabingwa BArani Afrika dhidi ya Mabingwa wa Afrika Kusini Mamelodi Sundown, utakaopigwa mapema mwezi Februari.

Kouki amesema mbali na kutarajia kucheza dhidi ya Simba SC (Februari 05), katika maandalizi yao wakiwa jijini Dar es salaam wangefurahi sana endapo wangepata fursa ya kucheza mchezo mwingine dhidi ya Young Africans.

“Unajua ndugu yangu mpira siyo siasa na ni mchezo wa wazi, sema hapa Tanzania mna uhasama wa Simba na Yanga nasi tunaongozwa na Mwenyeji wetu Simba,”

“Unajua Yanga ni wazuri unaona tu hata mechi zetu zilivyokuwa Dar na Khatoum licha ya kwamba tulishinda na kusonga mbele lakini tulipata ushindani thabiti na ukweli walituongoza umiliki wa mpira kote Dar na Khatoum.”

“Achana na hilo si unaona Yanga anaongoza ligi tena kwa pointi nyingi na bado yuko shirikisho na walishinda ugenini kwa upinzani mzuri? Ningefurahia sana ningepata mechi nae kwa sasa angenipa upinzani wa kutosha najua” amesema Kouki

Jana Alhamis (Januari 26) Kikosi cha Al Hilal kilicheza mchezo wake wa kwanza wa Kimataifa wa Kirafiki, Uwanja wa Azam Complex Chamazi dhidi ya Namungo FC.

Mchezo huo ulishuhudia miamba hiyo ikipata matokeo ya sare ya 1-1.

Al Hilal itacheza dhidi ya Azam FC Jumanne (Januari 31), Uwanja wa Azam Complex Chamazi, kisha itamaliza ziara yake nchini Tanzania kwa kucheza na Simba SC Jumapili (Februari 05), Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Amir Maftah: Sawadogo apewe muda kwanza
Rogaroga azusha mjadala akiomba nyimbo za Extra Musica mtandaoni