Katika tukio lisilokuwa la kiungwana, Afisa Elimu ya Msingi, Mohammed Msongo anatuhumiwa kumpiga makofi mwalimu wa shule ya msingi Ikombolinga iliyoko wilaya ya Chamwino, Peter Emma.

Akisimulia mkasa huo wa kusikitisha na kudhalilisha, mwalimu Emma aliwaambia waandishi wa habari kuwa alikutana na adhabu hiyo mbele ya walimu wenzake kwa sababu alichelewa kwa dakika 20 kufika katika semina ya mafunzo ya ‘KKK’ kwa ajili ya kuwafundisha watoto wa darasa la kwanza na darasa la pili.

Alisema kuwa licha ya kumueleza Afisa Elimu huyo kuwa alichelewa kwa kuwa alikuwa anakaa mbali na kwamba bado walikuwa hawajapewa fedha ya nauli, alipuuzwa na afisa habari huyo na kuambulia makofi.

“Tuliandika majina ya waliochelewa sijui tutalipwa au la maana tunatakiwa kulipwa Sh. 55,000 kwa kila siku na nauli lakini mpaka sasa hatujalipwa mimi sielewi kwa kweli nimefadhaika sana,” alisema mwalimu Emma. “Kama uongozi ni wa ubabe hivyo hakika kazi itakuwa ngumu sana kwani hali hii inavunja moyo,” aliongeza.

Hata hivyo, Afisa Elimu anayetuhumiwa kwa tukio hilo alipotafutwa alikana kumpiga makofi mwalimu huyo licha ya kukiri kuwa alimvuta shati kwa nyuma ili asiweze kujichanganya na wenzake waliokuwa wamewahi.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Chamwino, Richard Masimba alieleza kuwa ofisi yake haijapata taarifa yoyote kuhusu tukio hilo na kwamba endapo itapata taarifa hizo itachukua hatua za kinidhamu dhidi ya Afisa Elimu huyo.

Akizungumzia tukio hilo, Katibu wa Chama Cha Walimu wilaya ya Chamwino, James Puya alikiri kuwa amepokea taarifa za tukio hilo na kulaani vikali.

“Mimi nimepata taarifa za mwalimu kupigwa na nasema kama kiongozi wa CWT wilaya ya Chamwino kulikotokea hili tatizo naomba tume ya Haki za binadamu, Mkurugenzi na Utumishi kuingilia kati suala hili,” alisema Puya.

 

Picha: Msimu Mpya wa The Playlist ya Times Fm wazinduliwa kwa kishindo
Australian Open: Rafael Nadal Aushangaza Ulimwengu