Afisa Habari wa Klabu ya KMC FC Christina Mwagala amempiga Kijembe Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally, kufuatia Kampeni za kuhamasisha Mashabiki wa Klabu hiyo kwenda Uwanjani wakati wa Michezo ya Kimataifa.

Ahmed Ally amekua akifanya hivyo tangu alipotangazwa kuwa Mkuu wa Habari na Mawasiliano Simba SC mwanzoni mwa mwaka huu 2022, pale timu yao inapokua katika Uwanja wa nyumbani Benjamin Mkapa.

Christina amesema kwa kigezo cha ukubwa na umaarufu wa Simba SC, kiongozi huyo hakupaswa kutumia mbinu ya kutembea maeneo mbalimbali jijini Dar es salaam kuhimiza Mashabiki kwenda Uwanja wa Mkapa kuishangilia timu yao, bali alitakia kutumia mbinu nyingine ambayo ingeendelea kudhihirisha ukubwa wa klabu yao.

Amesema amekua akishangaa kuona baadhi ya Wadau wa Soka wakimpongeza Ahmed Ally na Jopo lake kwa kazi wanayoifanya ya kwenda mitaani kuhamasisha mashabiki kwenda kuishangilia timu yao inapocheza nyumbani kwenye michauno ya Kimataifa, kitu ambacho kwake haoni kama kina mantiki yoyote.

“Simba ina muda mrefu sana inashiriki ligi kuu Tanzania bara,hao hao wameshashiriki michuano ya Kimataifa, Lakini bado Afisa habari wao anazurura mtaani anatafuta mashabiki.

“Timu ambayo ina miaka na miaka, timu ambayo inajinasibu ina kila kitu, timu ambayo inajinasibu kwamba imesajili wachezaji kwa gharama, leo hii wewe uanze kuwafuata mashabiki mtaani kweli?”

“Hiki ni kitu ambacho (Ahmed Ally) mnatakiwa kumpa pole, hamtakiwi kumpa hongera” amesema Christina Mwagala

Mara ya mwisho Ahmed Ally alifanya Kampeni ya kuhamasisha Mashabiki wa Simba SC kabla ya mchezo wa Mkondo wa Pili wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika msimu huu 2022/23 dhidi ya Nyasa Big Bullet uliopigwa Jumapili (Septemba 18), Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Hersi Said: Young Africans ni mzigo mkubwa
Simba SC yahofia hujuma Angola