Nahodha msaidizi wa Azam FC, Agrey Moris, amesema hawatawaangusha mashabiki wa timu hiyo kwenye mchezo wa Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara (VPL) utakaofanyika katika Uwanja wa Taifa, Dar es Salaam

Mchezo huo utakaopigwa keshokutwa Jumatano saa 10.30 jioni,  unatarajia kuwa mkali na wa aina yake kutokana na timu zote mbili kuwa kwenye vita kali ya kuwania ubingwa wa ligi hiyo msimu huu.

Beki huyo wa muda mrefu wa Azam FC amewataka mashabiki kuondoa hofu kwani wachezaji wako katika morali ya hali ya juu na kila mmoja anajiandaa kwaajili ya kushinda mchezo huo.

Amesema licha ya ushindani kuwa mkubwa, ushindi wa 3-1 walioupata juzi dhidi ya Ndanda FC, umewaongezea nguvu zaidi ya kufanya vizuri katika mchezo huo.

“Hiyo inatupa morali zaidi ya kwenda kupambana kwa sababu sisi lengo letu ni kushinda mchezo huu na kujihakikishia tunaifukuzia Simba katika nafasi ya juu,” amesema Moris.

Tayari kikosi cha Azam FC kimeshaanza maandalizi kuelekea mchezo huo huku wachezaji wakiendelea kukaa kambini tangu ulipomalizika mtanange dhidi ya Ndanda, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kuzinasa pointi zote tatu kutoka kwa Simba.

Katika mchezo wa mzunguko wa kwanza uliofanyika Uwanja wa Azam Complex Septemba mwaka jana, timu hizo zilitoka suluhu.

Haji Manara: Okwi anaendelea vizuri
Zuma agoma kuachia madaraka