Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt.  John Magufuli leo Februari 27, amemuapisha Balozi Dkt. Bashiru Ally Kakurwa kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Ikulu jijini Dar es Salaam.

Akizungumza baada ya uapisho huo, Bashiru ambaye anajaza nafasi ya aliyekuwa Katibu Mkuu Kiomgozi, Hayati Balozi John William Kijazi aliyefariki dunia Februari 17, 2021, ameahidi kufanya kazi kwa juhudi, maarifa na weledi mkubwa ili kuwahudumia wananchi ikiwa ni njia ya kumuenzi aliyekuwa Katibu Mkuu Kiongozi Hayati Balozi John Kijazi.

Ikiwa ni  mara ya kwanza baada ya kuapishwa kushika wadhifa huo, Balozi Dkt. Bashiru amesema, kwa sasa majukumu yaliyo mbele yake ni kuhakikisha anasimamia utekelezaji wa ahadi za Rais kwa wananchi.

Balozi Dkt. Bashiru amesema kuwa awali alikuwa akisimamia Serikali itekeleze ahadi na Ilani ya CCM ya mwaka 2020-2025 lakini kwa sasa anaanza jukumu la kutekeleza ilani hiyo iliyobeba matumaini ya wananchi.

Aidha, Dkt. Bashiru ameahidi kuendelea kusimamia dhana ya mawasiliano baina ya serikali na wananchi ili kurahisisha utekelezaji wa masuala mbalimbali ya Serikali yanayowahusu wananchi.

Akizungumza katika hafla hiyo, Naibu Spika wa Bunge, Dkt. Tulia Ackson amesema Bunge litaendelea kushirikiana na Katibu Mkuu Kiongozi ili utekelezaji wa masuala mbalimbali yanayohusu Serikali na Bunge yaweze kufanyiwa kazi kwa haraka.

Naye Jaji Mkuu wa Tanzania, Profesa Ibrahimu Juma amemuahidi ushirikiano mkubwa katibu mkuu kiongozi katika utekelezaji wa majukumu yake.

Polisi Temeke wakamata magunia 49 ya bangi
Saudia yakanusha Salman kuhusika na kifo cha Khashoggi