Klabu ya Simba SC imedhamiria kupata Kocha Mkuu kutoka Bara la Afrika na kuachana na mpango wa Kocha kutoka Barani Ulaya, ili kutimiza mipango yake ya soka la ndani na Kimataifa.

Simba SC ipo kwenye mchakato wa kumapa Kocha Mkuu Mpya, baada ya kuachana na Kocha kutoka Serbia Zoran Maki, aliyeondoka klabuni hapo kwa makubaliano ya kuvunjwa kwa mkataba wake, mwishoni mwa mwezi uliopita.

Meneja wa Habari na Mawasilino Simba SC Ahmed Ally amesema Bodi ya Wakurugenzi inaendelea na mchakato wa kumpata Kocha Mkuu wa Kiafrika, baada ya kukubaliana kuachana na mpango wa kuajiri makocha kutoka nje ya Bara hilo.

Amesema Simba SC inaamini Makocha wa Kiafrika wana uwezo wa kuhimili mikiki mikiki ya soka la Afrika na mazingira yake, na itakua rahisi kwenda sambamba na misingi ya klabu yao, yenye njaa ya mafanikio Kimataifa.

“Tumeanza upya mchakato wa kusaka kocha wetu, malengo yetu ni kupata kocha Mwafrika au tukikosa tupate mwenye uzoefu na soka la Afrika. Kwa sasa timu ipo mikono salama ya kocha Mgunda”

“Simba SC inaamini Kocha wa kiafrika anajua mazingira ya soka la hapa, na ataendana na mazingira ya klabu, tunaamini katika hilo kwa sababu tutahitaji kuwa na kocha atakayekaa kwa muda mrefu ili aisaidie klabu kufikia mipango yake.” amesema Ahmed Ally akiwa kisiwani Unguja-Zanzibar

Simba SC tayari inahusishwa na mpango wa kutaka kuvunja mkataba wa Kocha Florent Ibenge anayeitumikia klabu ya Al Hilal ya Sudan, lakini imeripotiwa huenda ikakumbana na changamoto ya fedha ambazo zinatakiwa kulipwa kwa wababe hao wa mjini Khartoum, ili jambo lao litimie.

Kocha huyo kutoka DR Congo ana uzoefu mkubwa na soka la Afrika, huku msimu uliopita akiiwezesha klabu ya RS Berkane ya Morocco kutwaa Ubingwa wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Hujuma yahusishwa shambulio mabomba ya gesi
Privadinho: Hii ni chachu kwa vijana wa kitanzania