Uongozi wa Simba SC umethibitisha kufanya maboresho katika Kikosi chao kupitia Dirisha Dogo la Usajili, kwa kuzingatia mapendekezo ya Benchi la Ufundi linaloongozwa na Kaimu Kocha Mkuu Juma Ramadhan Mgunda.

Dirisha Dogo la Usajili litafunguliwa rasmi Desemba 15, ambapo Klabu zote za Ligi Kuu na Ligi Daraja la Kwanza, zitaruhusiwa kusajili wachezaji ambao wataboresha vikosi vyao.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema, kwa sasa wanasubiri ripoti maalum kutoka katika Benchi la Ufundi ili kufahamu wapi watakapoongeza nguvu kupitia usajili wa Dirisha hilo.

Aidha amesema wanashukuru wamemaliza salama mzunguuko wa kwanza wa Ligi Kuu na walichokipata sio haba, hivyo wanaamini Kocha Mgunda na Jopo lake watakuwa na sababu za kutosha kupitia ripoti yao, ili kuushawishi Uongozi kufanya jambo katika usajili.

“Tumemaliza Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi Kuu, tunamshukuru Mungu kwa tulichokipata, Dirisha Dogo linafunguliwa hivi karibuni na tutafanya maboresho kulingana na Benchi la Ufundi.” amesema Ahmed Ally

Simba SC imemaliza Mzunguuko wa Kwanza wa Ligi Kuu msimu huu ikiwa na alama 34, ikitanguliwa Young Africans yenye alama 35 lakini bado ina mchezo mmoja mkononi, huku Azam FC inayotarajiwa kumaliza mzunguuko huo kwa kucheza dhidi ya Polisi Tanzania leo Jumatatu (Desemba 05), ikiwa na alama 32.

Simba SC yaikaribisha Young Africans mezani
Papic: Kwa nini Simba SC, Young Africans haziamini wazawa?