Korea Kaskazini inaripotiwa kuchukua hatua kali za kuwaadhibu watu wanaodaiwa kusambaza au kutazama tamthilia maarufu iitwayo ‘Squid Game’.

Kwa mujibu wa Radio Free Asia, nchi hiyo imemhukumu kifo mtu mmoja kwa kusafirisha na kuuza nakala za mfululizo wa tamthilia hiyo ya Korea Kusini nchini humo.

Mwanafunzi wa shule ya sekondari aliyenunua nakala ya filamu hiyo amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kununua na kuonyesha kwa wenzie.

Wanafunzi wengine takribani sita wa shule ya sekondari ambao walitazama mfululizo wa tamthilia hiyo pia wamepatiwa adhabu ya miaka mitano ya kazi ngumu, huku wasimamizi wao, ambao ni walimu na viongozi kadhaa wa shule hiyo wakifukuzwa kazi.⁣

“Haya yote yalianza wiki iliyopita wakati mwanafunzi wa shule ya sekondari aliponunua kwa siri USB flash drive iliyokuwa na tamthilia hiyo ya Korea Kusini Squid Game na kuitazama na mmoja wa marafiki zake wa karibu darasani,” chanzo cha sheria katika jimbo la Hamgyong Korea Kaskazini kiliiambia RFA.

“Rafiki huyo aliwaambia wanafunzi wengine kadhaa, ambao walipendezwa, na kusambaziana Flash Drive hiyo.”⁣

Inaripotiwa kuwa hii itakuwa mara ya kwanza kwa nchi hiyo iliyojitenga kuchukua hatua kali kama hizo kwa watoto, chini ya sheria zake zinazoharamisha usambazaji wa filamu kutoka Korea Kusini, Marekani nk.

Tamthilia hiyo ambayo imeongozwa na muongozaji mahiri Hwang Dong-hyuk, ilijiwekea rekodi ya kipekee mtandaoni tangu mapema mwezi Septemba baada ya kuonyeshwa kwa mara ya kwanza kupitia mtandao wa Netflix huku ikijizolea maelfu ya wafuatiliaji Duniani kote.

Habari kubwa kwenye magazeti leo, Novemba 26, 2021
Madaktari watakiwa kuzingatia maadili ya Taaluma