Meneja wa klabu ya Middlesbrough Aitor Karanka de la Hoz amesema aliwahi kukataa ofa ya kuwa sehemu ya benchi la ufundi la Chelsea.
Karanka mwenye umri wa miaka 43, amesema ofa hiyo ya Chelsea ilielekezwa kwake wakati wa utawala wa Jose Mourinho, lakini aliona hakuna umuhimu wa kuendelea kuwa msaidizi, zaidi ya kujipanga na kuwa mkuu wa benchi la ufundi katika klabu yoyote.
Karanka amesema Mourinho aliwahi kumpigia simu na kumshawishi ili wafanye kazi kwa pamoja, lakini aliona bado kuna umuhimu wa kuendelea kujipanga zaidi akiwa katika benchi la ufundi la Real Madrid kama msaidizi.
Hata hivyo amekiri ofa hiyo ilikua kubwa sana kwake, kutokana na mazingira tofauti ya ligi, lakini bado akasisitiza aliona hakuna haja ya kwenda mahala ambapo ingekua changamoto ngeni katika ukufunzi wa soka.
“Nilitaka kuendelea kukaa Real Madrid kwa ajili ya kupata ujuzi zaidi, nilikua siifahamu vizuri ligi ya England kwa wakati huo na ndio maana ilikua rahisi kwangu kukataa kujiunga na Mourinho akiwa Chelsea.
“Japo ninakiri wazi kuwa ofa iliyokuja kwangu ilikua kubwa sana na haikuwahi kutokea tangu nilipoanza kukaa katika benchi la ufundi, lakini nilihofia kufanya kazi kwa mashaka.
Hata hivyo mwaka 2013 Karanka alifanikiwa kuondoka Real Madrid na kuelekea nchini England kuitikia wito wa klabu ya Middlesbrough, iliyokua ikishiriki ligi daraja la kwanza kwa wakati huo.
Aliitumikia klabu hiyo kwa miaka miwili akiwa kwenye ligi hiyo, na mwishoni mwa msimu uliopita alifanikiwa kuiwezesha kupanda na kucheza ligi kuu ya England.
Jana Karanka alikutana na Chelsea katika uwanja wa River Side na kikosi chake kilikubali kichapo cha bao moja kwa sifuri lililofungwa na Diego Costa.