Uongozi wa klabu ya Middlesbrough inayoshiriki ligi daraja la kwanza nchini England, huenda ukamtimua meneja wake Aitor Karanka, hata kama ikitokea kikosi chao kinafanikiwa kupanda daraja na kucheza ligi kuu msimu wa 2016-17.

Karanka ambaye aliwahi kuwa meneja msaidizi wa Real Madrid, wakati wa utawala wa meneja kutoka nchini Ureno, Jose Mourinho anapewa nafasi finyu ya kuendelea na kibarua chake huko Riverside Stadium kutokana na uwepo wa maelewano mabaya dhidi ya wachezaji wake.

Meneja huyo kutoka nchini Hispania anadaiwa kuwa mkali dhidi ya kikosi chake mara kwa mara, na imeripotiwa kwamba amekua akifanya kazi kwa kuzingatia maslahi yake binafsi.

Mara ya mwisho Karanka mwenye umri wa miaka 42, anadaiwa alifika mazoezini na kuwafokea wachezaji wake, hali ambayo ilimuumiza kila mmoja aliyekuwepo katika uwanja wa mazoezi siku hiyo, na katika mchezo uliofuata dhidi ya Charlton hakukaa kwenye benchi.

Mwenyekiti wa klabu ya Middlesbrough, Steve Gibson alipozisikia taarifa hizo hakufanya lolote zaidi ya kuahidi kulifanyia kazi kwa kuzingatia wakati utakapowadia.

Hata hivyo hatua hiyo ya mwenyekiti imetafsiriwa kama heshima kwa klabu ambayo inahitaji kupanda daraja katika kipindi hiki, hivyo inaaminiwa mwishoni mwa msimu kutakua na maamuzi magumu dhidi ya Karanka.

Alipoulizwa Karaka kuhusu mustakabali wake klabuni hapo, alidai kwamba anaheshimu mkataba wake uliosalia na muda wa miaka mitatu na hajali kitakachotokea mbele ya safari.

“Sitaki kusema nini kitakachotekea baadae, lakini ninaendelea kuheshimu mkataba wangu wa miaka mitatu.”

“Najitambua kama meneja wa klabu inayoshiriki ligi daraja la kwanza, ipo siku itatokea nitakua meneja wa klabu itakayoshiriki ligi kuu ya soka nchini England.” Alisema Karanka

Lakini pamoja na yote hayo kuzungumza na kutarajiwa kutolewa maamuzi magumu, bado haijafahamika ni kwa nini Karanka amekua na mtazamo tofauti dhidi ya wachezaji wake na kufikia hatua ya kuwabwatukia walipokua mazoezini.

Kesho kikosi cha Middlesbrough kitafahamu mustakabali wa kucheza ligi kuu msimu wa 2016-17, ama kuingia katika michezo ya hatua ya mtoano kwa kupambana na Brighton & Hove Albion.

Middlesbrough wanashika nafasi ya pili katika msimamo wa ligi daraja la kwanza wakiwa na point 88 sambamba na Brighton & Hove Albion hivyo mmoja kati ya wawili hao akipata point tatu muhimu atajiunga na Burnley ambao tayari wameshapanda daraja.

Na ikitokea matokeo ya sare yanapatikana katika mchezo huo Middlesbrough watanufainika na uwiyano mzuri wa mabao ya kufunga na kufungwa ambao unawaweka kwenye nafasi ya pili kwa sasa.

Thibaut Courtois Ashinikiza Bosi Wake Afukuzwe Stamford Bridge
Azam FC Wasuburi Ofa Ya Deportivo Tenerife