Baada ya kusambaa kipande cha video kinachomuonesha mwanaume mmoja akilia na ‘kujigalagaza’ chini akidai ‘Hamida amemuacha’, mtu mmoja anayedai kuwa ni ndugu wa mwanaume huyo amejitokeza na kueleza kuwa Hamida sio binadamu wa kawaida bali ni kiumbe asiyeonekana kwa macho ya kawaida (jini).

Mtu huyo aliyejitambulisha kwa jina la Abba, jana alifanya mahojiano na Clouds Media na kueleza kuwa yeye ni mganga wa jadi anayetumia majini mbalimbali kutibu watu, na kwamba Hamida ni moja kati ya viumbe hao.

Alisema Hamida hajawahi kuwa na uhusiano wowote na kijana huyo ambaye alimtambulisha kwa jina la Denis ambaye ni mjomba wake aishie mjini Iringa.

Kwa mujibu wa Abba, yeye anapokuwa anafanya kazi zake huwa viumbe hao wanamuingia na anatoa sauti zao. Hivyo, wakati Hamida amemuingia yeye na akawa anaendelea na kazi yake, Denis alimkejeli, kitendo ambacho kilisababisha Hamida amuadhibu.

“Akija anakuja na umbo na sura ya kwangu mimi, lakini akiongea inakuwa sauti ambayo ni ya kike na vitu vingine vyote, sasa jamaa (Denis) akawa kama anamkashfu. Kwahiyo yule kiumbe kusema kweli alikuwa amekasirika na akamwambia ‘ngoja nimalize kazi za watu halafu tutajua nini kitakachokutokea’. Na kweli yule jamaa, mimi nikiwa kama mtu, nikaja kukuta jamaa anagalagala anasema Hamida amemuacha,” alisimulia.

“Kwahiyo jambo lililomkuta yule sio kwamba alikuwa na mwanamke anayeitwa Hamida, lakini kwa jinsi alivyokuwa anaelezea sasa, baada ya mimi kuwa namhoji baadaye alipokuwa sawa, akaniambia kweli alikuwa anamuona mwanamke ambaye hajawahi kumuona – kipindi anagalagala, na sometimes alikuwa anaonesha hata vitendo,” aliendelea kusimilia.

Abba anadai kuwa alitumia takribani dakika 45 kumsaidia ndugu yake huyo ili arejee kwenye hali ya kawaida, na kwamba hata baada ya siku hiyo ilibidi atumie ‘kiumbe mwingine’ wa Kabila la Kimasai kumsaidia.

“Hata alipoamka bado alikuwa na maluelue, ikabidi nimuite kiumbe mwingine wa Kimasai, jamaa akapona na anaendelea na shughuli zake. Huyo jamaa yuko Iringa na tukio hili lilitokea wiki iliyopita mjini Iringa,” alisimulia.

Alisema kuwa mbali na kuwa na kiumbe Hamida ambaye ni wa Kisomali na huyo wa Kimasai aliyemtaja, huwa ana viumbe wengine anaowafuga ambao huwa wanamuingia na kufanya kazi. Anadai anaye mwingine ambaye ni ‘kijana msela’. Hapa akina dada angalieni msije mkakashfu yakawakuta na nyie mkaanza kulia ‘msela ameniacha’!

Jana, Dar24 Media ilifanya mjadala kuhusu hali hiyo ikiwa na imani kuwa ni tukio halisi la kuachwa na mpenzi. Mwanasaikolojia Justus alieleza kuwa wapo wanaume wengi wanaolia na kuumizwa na mapenzi,wengine hufikia hatua ya kutaka kujiua, ila tu hawaonekani. Hivyo, akatoa ushauri wa jumla wa jinsi gani unapaswa kufanya unapoachwa na mpenzi wako.

Maoni ya Mwandishi: Simulizi hili limejaa imani na ushirikina ambao ni vigumu kuwa na ushahidi wa moja kwa moja. Mwenyewe anasema kama anajua wengi hawataamini. Hivyo, uthibitisho wake bado unabaki kuwa nani anaamini nini! Japo maelezo ya ufafanuzi wa tukio yaliyotolewa yanaweza kuzua mjadala mwingine.

Ila Hamida, alivunja mitandao.

 

Video: JPM ahofia kung'olewa Urais, Prof. Kabudi atoboa siri ya kunusurika
Wakuu wa EU watia saini makubaliano ya Brexit

Comments

comments