Ni kweli nyaraka nyingi ndivyo zinavyoeleza, kuwa tabia au makosa ya binadamu ndiyo chanzo kikuu cha ajali kwa zaidi ya 70%, wakati vyanzo vingine vikipewa 30% zilizobaki.

Msimamo au mtazamo huu ni wa miaka ya 1970 hadi 1990 na ulilenga zaidi Kupunguza ajali kwa kurekebisha tabia ya dereva au mtumiaji wa barabara.

Ulijikita zaidi katika kuzuia ajali (crash prevention) kuliko kubaini vyanzo vya ajali (crash causes) kwa njia ya elimu, taarifa, na usimamizi wa sheria (education, information and police enforcement) pekee.

Mtazamo huu haukuzingatia ukweli kwamba ajali sio matokeo ya chanzo kimoja tu bali muunganiko wa vyanzo vingi na hivyo mtazamo huu ulidharau au kuzipa uzito mdogo sababu nyingine kama vile ubovu wa magari na ubovu wa barabara.

Ndio maana utaona miundombinu inapewa 8% tu, na ubovu wa magari unapewa 16% tu na tafsiri yake ni kwamba Polisi hawafanyi kazi, hawakagui magari wala hawadhibiti tabia za watumiaji wa barabara.

Polisi wameendelea kuimba wimbo huu huku wakilalamika kuachiwa huo mzigo peke yao, lakini wakati mwingine wakisaidiwa baadhi wamekuwa wakiona kama wanaingiliwa majukumu, kwamba usalama barabarani ni wa Jeshi la Polisi Pekee.

Dunia sasa imetambua kuwa mtazamo huo wa kale (traditional approach) umefeli kuleta matokeo yanayokusudiwa, hivyo imebadili mtazamo kutoka kumuangalia mtu hadi kuangalia usalama barabarani kama mfumo (system), ambapo katika mfumo huo kila chanzo kinachangia ajali kwa 100%.

Waasisi wa mtazamo huu ni Sweden (Vision zero), Uholanzi(Sustaible Safety), na OECD(Safe system), na  umekubalika na Umoja wa Mataifa huku mfumo mpya wa usalama barabarani ukijikita katika misingi kwamba ni vigumu kubadili tabia ya binadamu ili kupunguza ajali.

Mtazamo huu pia unatambua kuwa ni jambo lisilowezekana kuzuia ajali zote hivyo tujikite zaidi kwenye kupunguza madhara ya ajali na hili linawezekana kwa kutengeneza mfumo wa barabara unaoruhusu makosa ya kibinadamu huku ukipunguza madhara.

Mfumo wa barabara sharti uvumilie makosa ya binadamu (barabara zinazosamehe), gari sharti lisamehe makosa ya binadamu (gari linalosamehe), na haya yanawezekana kwa kuanzia na kujikita zaidi kwenye uundaji wa magari (vehicle design) na usanifu wa barabara (road design).

Ikiwa gari halikuundwa vizuri kusamehe au kuondoa makosa ya dereva, likija Tanzania hata likaguliwe vipi litasababisha ajali tu kwani lina makosa ya kimuundo. Vivyo hivyo, hata upange askari kila mita 1, kama barabara haikusanifiwa na kujengwa vizuri kwa viwango ajali zitatokea tu na zitasababisha madhara makubwa.

Kwa ufupi, “System designers are responsible for overall safety performance of the system”, yaani waundaji wa mfumo wanawajibika na ufanisi wa ujumla wa mfumo.

Nyumbani una mtoto mdogo wa mwaka 1 hadi 2, ni mtundu sana hasikii anachezea pasi, nyanya za umeme, visu, nyembe, anapanda juu ya meza, nk. Na kila siku wee huachi kumkemea, wakati mwingine unamfinya analia lakini anaendelea na ana makovu mbalimbali.

Je, unadhani mbinu ya kumkemea pekee na kumchapa inatosha? Je, unadhani mbinu ya kumfungia ndani pekee ndio suluhu ya kudumu? Vipi, ukijaribu kuondoa hivyo vitu vya hatari kwake wakati huo huo unaendelea kumkemea au kumzuia? Ondoa meza za vioo, ficha wembe, kisu, nk, yes mtoto atendelea kuwa mtundu ataanguka, lakini je ataumia kama ambavyo angedondokea meza ya kioo au kisu?

Kutoka kwenye ukurasa wa Facebook wa RSA Tanzania.

Itaendelea…….

Habari Kuu kwenye magazeti ya leo Juni 4, 2023
Aliyevua nguo madhabahuni atoa sababu, akamatwa