Mtu mmoja mkazi wa Kashai Manispaa ya Bukoba Mkoani Kagera amekutwa amejinyonga kwa kamba ya katani hadi kufa nyumbani kwake kwa kile kinachodaiwa kuwa ni kutokana na hali ngumu ya maisha baada ya kugundulika anaishi na Virusi vya Ukimwi.

Marehemu huyo aliyetambulika kwa jina la Salvatory Rweyemamu ambaye ameacha Mke na watoto watatu amekutwa akiwa amefariki katika chumba chake alichokuwa akiishi Januari 6, 2019 majira ya saa tatu asubuhi mara baada ya kijana wa kaka yake alipokwenda kumjulia hali.

Imeelezwa na majirani wa marehemu kuwa, mara baada ya kijana huyo kufika nyumbani kwa marehemu Salvatory, alibisha hodi kwa muda mrefu bila kujibiwa, na hapo ikabidi kuulizia taarifa zake kwa majirani, hali hiyo ya sintofahamu ikapelekea majirani kuamua kuchungulia dirishani ndipo walipogundua kuwa amefariki na mwili wake ulikuwa ukining’inia juu ya dari.

Kutokana na hali hiyo taarifa zilitolewa kwa Mwenyekiti wa Kijiji, Victor Herman na kufika eneo la tukio mara moja kisha naye akalijulisha Jeshi la Polisi ambapo baada Polisi kuwasili eneo la tukio, ndipo waliuteremsha mwili wa marehemu kuutoa katika kitanzi, na katika kupekua pekua ndani wakakutana na ujumbe ulioachwa na marehemu ukisomeka kuwa;

“Nimeamua kujiua maisha yamekuwa magumu, Ukimwi noma, baiskeli yangu ipo kwa fundi wapewe wanangu”

Kwa upande wake mdogo wa marehemu, Bernadetha Rweyemamu (30) kwa masikitiko makubwa akisimulia kuhusu msiba wa marehemu kaka yake amesema kuwa, kwa wiki tatu zilizopita marehemu alikuwa akijihisi kuumwa mara kwa mara, na baada ya kupimwa aligundulika kuwa ni muathirika wa VVU, hali iliyomfanya aanze kuzorota kiafya na kuwa mtu wa mawazo sana.

Ameongeza kuwa, kwa kipindi chote hicho hadi umauti unamfika marehemu Salvatory alikuwa akiishi peke ake na akiendelea na shughuli zake za kila siku za uchomeleaji vyuma.

Kutokana na kifo hicho baadhi ya marafiki na jirani wa marehemu hawakusita kuzungumzia tukio hilo huku, Andrew John akidai kuwa marehemu alikuwa rafiki yake na wakifanya shughuli zao pamoja katika karakana yao ya uchomeleaji, na kwa mara ya mwisho waliachana juzi akiwa katika hali ya kawaida kama siku zote japo alionekana mwenye mawazo sana.

Naye, Denice James (27) jirani wa marehemu alipokuwa akiishi amenukuliwa akisema kuwa Marehemu Salvatory (Babu) alikuwa mtu wa kujifungia ndani mara kwa mara na wakati mwingine angeweza kujifungia kwa kipindi cha siku tatu bila kutoka nje, ingawaje aliishi kwa mahusiano mazuri yeye na mjiarni zake wengine.

Mwili wa marehemu umechukuliwa na jeshi la polisi ambapo mkuu wa upelelezi wilaya Bukoba amethibitisha kutokea kwa tukio hilo na tayari umehifadhiwa chumba cha maiti katika Hospitali ya Rufaa Bukoba ukingoja taratibu za mazishi.

Marehemu ameacha Mke na watoto watatu huku akisisitiza Baiskeli yake ipo kwa fundi wapewe watoto wake.

Video: Makonda kuendeleza utekelezaji sera ya elimu bure Dar
Kufuru za Diamond siku ya ndoa yake, Tanasha akazia