Baadhi ya akina mama Wilayani Mufindi, wameiomba serikali kuwapa mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, ili waweze kujiendeleza katika biashara zao na kujiinua kiuchumi na kuacha kukopa mikopo umiza.

Akinamama hao wamesema hayo mbele ya Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi, Daniel Chongolo na kueleza kuwa wamekuwa hawapati mikopo hiyo na badala yake wanakopa mikopo ya kausha damu na kuwafanya kushindwa kurejesha mikopo hiyo na kuishia kutelekeza familia na kukimbia madeni.

Mmoja wa akina mama hao na Mjumbe wa CCM shina namba 3 kata ya Boma, Mwajuma Mbata alisema kuwa mikopo hiyo inatolewa kwa masharti ya kutengeneza vikundi katika makundi maalum ya wajasiliamali wadogo, lakini wanaopata mikopo hiyo ni wale wenye uwezo wa kukopa benki.

Amesema, “kukosekana kwa mikopo hiyo kunatufanya tunajiingiza katika mikopo ya moto, maarufu kama kausha damu na tukishindwa kulipa tunaachika katika ndoa zetu na kutelekeza watoto, wanaopata mikopo hiyo ni wale ambao wanauwezo wa kukopa katika mabanki na ndio baadaye tunarudi kuomba mikopo kausha damu kwao ambayo inatuumiza.”

Ameongeza kuwa, wanaiomba serikali iwaangalie wajasiliamali wadogo kwa kuwapunguzia masharti hasa katika dhamana, ili wanapojiunga katika vikundi hivyo waweze kuipata mikopo hiyo itakayowasaidia kujiinua kiuchumi.

Akijibu hoja hiyo, Chongolo alisema Serikali ilifanya maamuzi ya kusitisha mikopo ili kutengeneza utaratibu mzuri kwani lengo lake ni kuwawezesha vijana walemavu na akina mama kujikwamua kiuchumi na utaratibu huo utakuwa umekamilika mwezi Agosti ambao utakuwa na tija kwa vijana na kiuchumi.

Title: Meridianbet Yazindua Duka Jipya Ubungo-Kibangu
Chama afichua kilichoikwamisha Simba SC