Mwanamuziki mashuhuri na mzaliwa Senegal ambaye pia ni raia wa Marekani mwekezaji na mhisani Aliaune Damala Badara Thiam, maarufu Akon amewasili nchini Uganda asubuhi ya leo Ijumaa, kwa ziara ya kibiashara.

Hii inafuatia ziara ya hivi karibuni ya mkewe, Rozina Negusir mnamo Januari mwaka huu.

Negusir alikutana na Rais Museveni na wakajadili miradi tofauti ya uwekezaji ambayo inaweza kufanywa, kulingana na Wizara ya Mambo ya nje.

Akon alipokelewa na Abbey Walusimbi, mshauri mwandamizi wa Rais katika masuala ya ya raia walio nje ya nchi hiyo, mwanamuziki Eddie Kenzo, maafisa kutoka Wizara ya Mambo ya nje, Bodi ya Utalii ya Uganda, na Sheik Ramadhan Mulindwa kutoka Baraza Kuu la Waislamu la Uganda.

Kwa mujibu wa Wizara ya Mambo ya Nje ya Uganda, katika ziara yake hii Akon pia anatarajiwa kukutana na Rais Museveni kujadili fursa tofauti za uwekezaji katika sekta mbali mbali za Nishati, utalii, maendeleo ya miundombinu, miongoni mwa nyingine.

Mwaka 2018 Akon alitangaza mpango wa kujenga jiji la kisasa kwa kima cha dola bilioni 6 nchini Senegal kwa jina “Akon City”.

Mradi huo unaoungwa mkono na serikali ya Senegal utakuwa na hoteli za kifahari za watalii, studio za muziki, maduka makubwa ya bidhaa na vivutio vingine.

Polisi: Hatujapiga marufuku ibada za sikukuu ya Pasaka
NCCR Mageuzi yaungana na CHADEMA, yasusia uchaguzi