Inaelezwa kuwa Mabingwa wa Soka nchini Sudan klabu ya Al Merrikh wameonesha nia ya kutaka kumsajili mlinda mlango chaguo la kwanza la Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Aishi Salum Manula.

Al Merrikh ambao walikuja nchini juma lililopita kucheza mchezo wa mzunguuko wanne wa Ligi ya Mabingwa Barani Afrika hatua ya Makundi dhidi ya Simba SC, wanahusishwa na mpango huo kufuatia kupendezwa na kiwango cha Manula kwenye michuano ya kimataifa.

Kocha Mkuu wa Al Marriekh Lee Clark anadaiwa amekutana na Rais wa klabu hiyo Adam Sudacal na kumshawishi kumsajili Manula, kwa kuamini ataweza kumsaidia kwenye michezo ya Ligi Kuu ya Sudan na michuano ya kimataifa kwa msimu ujao wa 2021/22.

Taarifa kutoka nchini Sudan zinadai kuwa, Rais wa klabu hiyo Adam Sudacal ameonesha kukubaliana na ombi la kocha wake, na wakati wowote huenda akatuma ofa Simba SC ambayo inakadiriwa kufikia dola za kimarekani 100,000 sawa na milioni 230 kwa pesa za Tanzania,

Hata hivyo haijafahamika kama Simba SC wataikubali ofa hiyo endapo itatumwa, kutokana na ubora na uwezo wa mlinda mlango wao Aishi Manula ambaye bado hajaonja chungu ya kufungwa kwenye michezo ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika, hatua ya makundi, tangu ilipoanza mwezi Februari.

Baada ya klabu ya Simba kumuajili kocha mpya wa makipa raia wa Brazil Milton Nienov kumefanya kiwango cha mlinda mlango huyo kuimarika zaidi ukilinganisha na msimu uliopita.

Msimu huu Manula ameweka rekodi katika michuano ya klabu bingwa Africa Mara baada ya kuruhu goli 1 katika michezo 7, goli ambalo alifungwa katika mchezo dhidi  Platinum FC.

Msuva aahidi kupambana Equatorial Guinea
Rais Mwinyi: Kiongozi kama Magufuli ni nadra kupatikana