Kiungo Mkabaji kutoka nchini Cameroon na klabu ya AS Arta Solar ya Djibouti, Alex Song anaamini Simba SC ina nafasi kubwa ya kuuza wachezaji wengi nje ya Tanzania katika kwa kipindi kifupi.

Song ambaye kwa sasa yupo Dar es salaam sambamba na kikosi cha Arta Solar kilichoweka Kambi ya maandalizi ya msimu mpya, amesema kikosi cha Simba kinaundwa na wachezaji wengi wenye vipaji na kwamba kama watakuwa wanajituma zaidi muda utaongea kabla ya kupata nafasi ya kucheza soka la kulipwa katika klabu kubwa za nje.

AS Arta/Solar 7 inatarajia kucheza mchezo wa Kimataifa wa Kirafiki dhidi ya Simba Septemba 03, Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

Song amesema halifahamu vizuri soka la Tanzania ila alikuwapo katika Kilele cha Simba Day na kuona jinsi Watanzania wanavyopenda soka na timu yao.

Amesema kuhusu wachezaji wa Simba aliowaona siku hiyo wakati wakicheza mchezo wa kirafiki dhidi ya St. George ya Ethiopia, ni wazuri na anaamini wengi wao wana nafasi ya kucheza soka nje ya Afrika na kwamba kikubwa wanatakiwa kupambana na kujituma.

“Sijawahi kulifuatilia soka la Tanzania, sherehe za Simba nilifanikiwa kushuhudia mchezo wao wa kirafiki dhidi ya St. George ya Ethiopia, kilichonivutia ni kuona mashabiki wengi kujitokeza na kujaza uwanja, hii ni ishara ya Watanzania kupenda cha kwao, lakini nimeona wachezaji wazuri na wakijituma zaidi watapata nafasi ya kucheza soka nje ya Afrika.

“Nina imani kufika kwetu kucheza soka Ulaya kunachangiwa na kuwasikiliza waliotuzidi, kuwa makini, kujituma, kufuata yale tunayopewa na kocha pamoja na kuhakikisha unathamini ile nembo ya jezi unayotumikia, ndiyo sababu kubwa ambayo imetufanya kufanikiwa na kucheza klabu mbalimbali Ulaya,” amesema Song.

Kuhusu kurejea Afrika na kucheza ndani ya kikosi cha timu hiyo inayoshiriki Ligi Kuu ya Djibouti, amesema ni kwa sababu ya kutaka kuendelea kuacha uzoefu na kutoa somo kwa baadhi ya wachezaji vijana ili kufikia malengo yao.

“Huku ukanda wetu wa Afrika ni nchi chache sana ambazo wachezaji wanatoka katika kituo cha soka, wengi wao hawana misingi ya soka kuanzia chini sasa kuwapo kwangu hapa katika Klabu ya AS Arta Solar ni kutoa somo kwa vijana na kuwaeleza ni namna gani ya kufikia malengo yao ya kucheza soka kama ilivyo kwangu,” amesema Song ambaye katika klabu hiyo yupo na nyota wa zamani wa Chelsea, raia wa Ivory Coast, Solomon Kalou.

Kocha Matola ataja siri za kuibamiza Asante Kotoko
Kenya: IEBC, Wapiga kura waingia kazini