Aliyekua kiungo wa klabu ya Arsenal Alexander Hleb, kwa mara ya kwanza amejutia hadharani, hatua ya kuondoka kaskazini mwa jijini London na kutimkia FC Barcelona mwaka 2008.

Hleb amejutia hatua hiyo akiwa jijini London, alipokwenda na kikosi cha klabu yake ya BATE Borisov kwa ajili ya mchezo wa Europa League dhidi ya Chelsea uliochezwa usiku wa kuamkia leo, na The Blues kupata ushindi wa mabao matatu kwa moja.

Kiungo huyo kutoka nchini Belarus amesema, alipoondoka Arsenal anaamini mashabiki wengi hawakupendezwa na maamuzi yake, na yeye binafsi alilitambua suala hilo baada ya kupata wakati mgumu wa kujumuishwa kwenye kikosi cha kwanza cha FC Barcelona chini ya meneja Pep Guardiola kwa wakati huo.

“Najua niliwakwaza mashabiki wa Arsenal, walihitaji huduma yangu kwa miaka mingine mingi, lakini niliharakisha kuondoka.”

“Maamuzi yangu ya kujiunga na FC Barcelona hayakua sahihi, sikufurahia maisha ndani ya klabu hiyo ya Hispania,” Alisema kiungo huyo mwenye umri wa miaka 37.

“Nilipoteza muda mwingi nikiwa FC Barcelona, ningelijua ni bora ningelibaki Arsenal, nilikua na uhakika wa kucheza mara kwa mara chini ya Arsene Wenger.”

Hleb alijiunga na FC Barcelona kwa ada ya Pauni milioni 12, na kwa wakati wote alipata nafasi ya kucheza kwenye kikosi cha klabu hiyo mara 19.

Baada ya kukabiliwa na changamoto ya kushindwa kuwa sehemu ya kikosi cha kwanza, Hleb aliuzwa kwa mkopo kwenye klabu ya Stuttgart Ujerumani kisha Birmingham ya England na baadae Wolfsburg ya Ujerumani, kabla ya kutimkia Krylia Sovetov Samara ya Urusi mwaka 2012.

Klabu nyingine alizowahi kuzitumikia ni BATE Borisov (2012–2013), Konyaspor (2014) , Gençlerbirliği (2015), BATE Borisov (2015), Gençlerbirliği (2016), BATE Borisov (2016), Krylia Sovetov Samara (2017) na BATE Borisov (2018).

Serikali yamtaka Wema ajieleze
Sakata la vilipuzi nchini Marekani bado kitendawili