Mshambuliaji wa Arsenal Alexis Sanchez yupo kwenye msukosuko wa kufikishwa mahakamani, kufuatia kesi ya kukwepa kulipa Kodi wakati akiitumikia FC Barcelona ya Hispania kwa kipindi cha mwaka 2012 na 2013.

Tuhuma hizo zimeripotiwa na Gazeti la Spain El Periodico, ambalo limedai Sanchez mwenye mwenye umri wa miaka 27, atafikishwa mahakamani kwa tuhuma za kutolipa Kodi kutokana na mapato ya umiliki wa matangazo yaliyomuhusu kwa kipindi cha mwaka 2012 na 2013.

El Periodico limedai kuwa, Sanchez alihamisha umiliki wa matangazo yake kwenye kampuni iitwayo Numidia Trading ambayo aliimiliki kwa asilimia 99 lakini alificha umiliki huo.

Awali umiliki wa matangazo ya mshambuliaji huyo kutoka nchini Chile ulikuwa chini ya kampuni ya iitwayo Inversiones Alsan anbayo pia aliimiliki kwa asilimia 99.

Lakini imedaiwa Kampuni hizo hazikuwa na sifa halisi ya kuitwa kampuni.

Pia inadaiwa kuwa mwaka 2011, Sanchez alisaini mkataba na FC Barcelona ambao uliainisha umiliki wa haki za matangazo ya biashara zake.

Waendesha mashtaka nchini Hispania wamedai “Numidia” ni kampuni iliyobuniwa ili kukwepa kulipa kodi na huo ndio msingi wao wa kufungua mashtaka dhidi ya mshambuliaji huyo.

Alexis Sanchez si mchezaji wa kwanza aliehusiana na FC Barcelona kukabiliwa na tuhuma za ukwepaji wa kodi katika miaka ya hivi karibuni.

Wengine waliokumbwa na misukosuko hiyo ni Lionel Messi, Javier Mascherano, Samuel Eto’o na Adriano.

Serikali yamjibu Mbowe, 'hatufanyi kazi kwa miujiza'
Bakora Ya FA Yamchapa David Moyes