Washika bunduki wa kaskazini mwa jijini London (Arsenal FC) watashuka dimbani mwishoni mwa juma hili kuikabili Leicester City katika mchezo wa kwanza wa ligi ya nchini England msimu wa 2017/18, bila ya mshambuliaji wao kutoka nchini Chile Alexis Sanchez.

Meneja wa Arsenal Arsene Wenger, amethibitisha taarifa hizo katika mkutano na waandishi wa habari mapema hii leo, kwa kusema atashindwa kumtumia Sanchez mwishoni mwa juma hili, kutokana na majereha aliyoyapata akiwa katika mazoezi.

Wenger amesema mshambuliaji huyo pia ataukosa mchezo wa pili wa ligi kuu ya England ambapo kikosi chake kitasafiri kuelekea Stoke On Trent kwa ajili ya kuwakabili Stoke City Agosti 19.

“Alipatwa na maumivu ya misuli ya tumbo akiwa katika mazoezi siku ya jumapili asubihi, alifanyiwa vipimo siku mbili zilizopita na ameshauriwa kupumzika kwa kipindi cha majuma mawili.” Amesema Wenger

Sanchez, ambaye alimaliza msimu uliopita akiwa mfungaji bora wa kikosi cha Arsenal kwa kufunga mabao 24, anahusishwa na taarifa za kuwaniwa na matajiri wa jijini Paris nchini Ufaransa Paris St Germain (PSG), lakini Wenger ameendelea kusisitiza mchezaji huyo atasalia Emirates Stadium.

Mkataba wa Sanchez wa kuitumikia The Gunners, utafikia kikomo mwishoni mwa msimu huu, na mpaka sasa haijaeleweka kama atasaini mkataba mpya wa kuendelea kuitumikia klabu hiyo, ambayo mwishoni mwa juma lililopita iliichapa Chelsea kwa changamoto ya mikwaju ya penati nne kwa moja katika mchezo wa Ngao Ya Jamii, baada ya kwenda sare ya bao moja kwa moja ndani ya dakika 90.

Rafael Benitez: Sifurahishwi Na Usajili Wa Newcastle Utd
AS Roma: Mpaka Kieleweke Kwa Riyad Mahrez