Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) kwa nyakati tofauti amekutana na kufanya mazungumzo na Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Denmark, Finaland na Norway ambao wamekuja nchini kuhudhuria Mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi za Afrika na Nordic unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Viongozi hao wamezungumzia na kukubaliana  kuendelea kuimarisha mahusiano mazuri ya kirafiki na kihistoria yaliyopo baina ya nchi hizo.

Katika mazungumzo hayo Prof. Kabudi amezieleza nchi hizo kuhusu msimamo wa Serikali ya Tanzania katika kujiimarisha kiuchumi kupitia ukusanyaji wa mapato ya ndani ili iendelee kutoa elimu bure na bora kwa watoto wa kitanzania, huduma bora za afya kwa watanzania, kuwezesha upatikanaji wa maji safi na salama kwa wananchi wote na kufikisha huduma za Nishati kwa watanzania wote hasa wa vijijini.

Amesema kwamba Tanzania itaendelea kutoa kipaumbele kwa siasa za maendeleo ili kuhakikisha azma ya kuwa nchi ya uchumi wa kati na wa viwanda inafikiwa.

“Tanzania haiangalii Siasa za nguvu, tunaangalia Siasa za kuletea wananchi maendeleo, na kwa mpango huo tutaendelea kuimarisha ukusanyaji wa mapato yetu ya ndani na kumfanya kila mtanzania kulipa kodi ili tuendelee kutoa elimu bure ya msingi na sekondari kwa watoto wa Kitanzania, kuboresha huduma za afya hadi vijijini, upatikanaji wa maji safi na salama na kuhakikisha huduma za nishati ya umeme zinawafikia watanzania wote hadi wa vijijini,” alisema Prof. Kabudi.

Amewahahakishia mawaziri hapo kuwa Tanzania itaendelea kuheshimu makubaliano ya Kimataifa hasa katika suala la wakimbizi na kuwafanya watu wanaokuja kutafuta hifadhi za kisiasa nchini kwetu wana pata hifadhi hizo.

Akizungumza alipokutana na Prof. Kabudi Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark Mhe. Jeppe Koffod amemuhakikishia Prof. Kabudi Serikali ya Denmark itaendelea kuiunga mkono Tanzania katika jitihada zake za kuimarisha huduma za jamii kama vile utoaji wa elimu bure, huduma za afya na maji salama.

Pia amesisitiza kwamba wataendelea kuunga mkono mpango wa utoaji wa elimu ya ufundi nchini na kuwafanya vijana wa kike na wa kiume Nchimbi kushiriki katika harakati za ujenzi wa taifa lao.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Finland Mhe. Pekka Haavisto ameahidi nchi yake kuendelea kuisaidia Tanzania katika maeneo ya misitu, utawala bora, ukusanyaji mapato, haki za binadamu na Tehama.

Amesema Finland pia itaendelea kuisaidia Tanzania kwenye Elimu kwakuwa Elimu imekuwa na mchango mkubwa na hivyo kutoa viongozi wa baadaye.

Naye Waziri wa Mambo ya Nje wa Norway Mhe. Ine Eriksen Soreide ameipongeza Serikali ya Tanzania kwa kazi kubwa inayofanya ya kupambana na rushwa na ufisadi na hivyo kuongeza imani ya Norway kuwezesha zaidi nchini. Aidha, ameahidi kuwa nchi yake itaendeleza Ushirikiano wake na Tanzania.

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Prof. Palamagamba John Kabudi (Mb) akimkabidhi zawadi ya kamusi ya Kiswahili – Kiingereza Waziri wa Mambo ya Nje wa Denmark Mhe. Jeppe Kofod wakati walipokutana jijini Dar es Salaam

Prof. Kabudi pia amekutana na Waziri wa Mambo ya Nje wa Msumbiji Mhe. Jose Pacheco na kujadiliana mambo mbalimbali ikiwemo kuimaraisha mahusiano baina ya Msumbiji na Tanzania.

Mawaziri hao wako nchini kuhudhuria mkutano wa 18 wa Mawaziri wa Mambo ya Nje wa nchi 29 za Afrika na Nordic unaofanyika jijini Dar es Salaam.

Jafo azipa ujumbe AZAKI kuhusu mafanikio ya Serikali
Makonda afunguka alivyoipania Wasafi Festival

Comments

comments