Klabu ya Liverpool imekamilisha usajili wa mlinda mlango kutoka nchini Brazil Alisson Becker, kwa kumsainisha mkataba wa miaka mitano akitokea AS Roma ya Italia.

AS Roma nao wamethibitisha kukamilika kwa dili hilo, ambalo limeigharimu Liverpool kiasi cha Euro milioni 62.5 sawa na Pauni milioni 55.9, na kiasi kingine cha pesa Euro milioni 10 sawa na Pauni milioni 8.95 kitaongezwa kutokana na kiwango cha mlinda mlango huyo mwenye umri wa miaka 25.

Usajili wa Alisson unaweka rekodi mpya katika ligi ya England, kwa kuivunja rekodi iliyokua inashikiliwa na mlinda mlango wa mabingwa wa ligi hiyo Manchester City Ederson Santana de Moraes, aliyesajiliwa kwa gharama ya Pauni milioni 34.7 akitokea Benfica msimu uliopita.

“Ninafuraha isiyo kifani, ndoto zangu za kuvaa jezi ya klabu ya Liverpool zimekua kweli,” alisema Alisson alipohojiwa na mwandishi wa tovuti ya liverpoolfc.com.

Alisson amesajiliwa klabuni hapo kuchukua nafasi ya aliyekua mlinda mlango chaguo la kwanza Loris Karius, ambaye alifanya madudu katika mchezo wa fainali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Real Madrid mwezi Mei.

Mlinda mlango mwingine ambaye atapata changamoto ya kuwania nafasi kwenye kikosi cha kwanza cha Liverpool baada ya kusajiliwa kwa Alison ni Simon Mignolet.

Kwa upande wa meneja wa Liverpool Klopp alizungumza maneno machache baada ya usajili wa Alison kukamilishwa: “Tumefanikisha tulilokua tunalihitaji, kwa zaidi ya juma moja tulishughulikia usajili wa mlinda mlango, tumefanikiwa, sasa tunaingia katika mapambano ya msimu ujao tukiwa kamili.

“Kulikua na ulazima wa kufanya usajili wa mlinda mlango, kutokana na mapungufu tulionayo katika nafasi hiyo, ninaamini kila mdau anaehusika na Liverpool atakua ameridhishwa na usajili wa Alison.

Alisson alicheza michezo 49 akiwa na AS Roma msimu uliopita, na alionyesha maajabu wakati wa mchezo wa nusu fanali wa ligi ya mabingwa barani Ulaya dhidi ya Liverpool msimu uliopita, uliomalizika kwa majogoo wa jiji kuibuka na ushindi wa jumla wa mabao 7-6.

Alisson pia ni chaguo la kwanza katika kikosi cha timu ya taifa ya Brazil, na alicheza michezo yote ya timu hiyo, wakati wa fainali za kombe la dunia, zilizomalizika nchini Urusi mwishoni mwa juma lililopita.

Video: Kauli ya Obama yakamata, Mbegu za matunda tiba nguvu za kiume
Habari kubwa katika magazeti ya Tanzania leo Julai 20, 2018